Parachichi ni tunda muhimu kwa kila mlo, kwa ujumla litakufanya uwe vizuri kiafya kwa muda mrefu.

Tunda hili lina vitamini B na Folic Acid ambayo kitaalam pia inaaminika kuwa na uwezo wa kuondoa msongo wa mawazo (stress). Zaidi, tunda hili lina protini, fat (mafuta) na Vitamini E. Utajiri wa virutubisho hivi ni moja kati ya sababu za watalaam kupendekeza kuwa tunda hili lisikosekane kwenye kila mlo wako angalau mara moja kwa siku. Nikudokeze tu kuwa ingawa matunda mengi husaidia kuongeza kinga ya mwili, tunda hili lina ukwasi wa aina yake katika zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Fausta Akech, mtaalam wa afya ya chakula kutoka kituo cha Health U, parachichi lina faida nyingine kubwa katika mfumo wa chakula wa binadamu ikiwa ni pamoja na kusaidia katika kulainisha choo huku ikizuia kuhara. Ndio!

“Hii ndio sababu parachichi ni tunda linaloshauriwa zaidi hasa kwa watu wenye matatizo ya mfumo wa chakula pamoja na ugumu wa haja. Zaidi parachichi hupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya tumbo ,” Akech ameeleza.

Kwa wajawazito

Akech anaeleza kuwa parachichi ni muhimu sana kwa mwanamke mwenye ujauzito kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha folic acid; na ni muhimu katika kurekebisha seli za mwili na kusaidia afya ya uzazi hasa mapigo ya moyo ya mama na mwana. Ulaji wa parachichi humsadia afya ya ubongo pamoja na mfumo wa fahamu wa mtoto mchanga.

Afya ya Ubongo:

Parachichi limebainika kuwa na virutubisho vinavyoboresha afya ya ubongo kwa kusaidia mzunguko mzuri zaidi wa damu kwenda kwenye ubongo, hivyo kuufanya ubongo kuwa na utulivu zaidi. Pia, ina vitamini E ambayo inasaidia kuulinda ubongo dhidi ya uharibifu na kiharusi.

Afya ya Moyo:

Watu wengi hawapati mlo bora wenye potassium hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata shinikizo la damu. Parachichi ni tunda litakalokusaidia kurekebisha mfumo wa damu na kupunguza hatari ya kupata matatizo ya figo pamoja na magonjwa mengine ya moyo.

“Kwa kusisitiza tu, parachichi lina vitamini E ambayo inapunguza ‘cholesterol oxidation’ ambayo inaweza kusababisha mshtuko wa moyo na kiharusi. Oleic acid iliyo kwenye parachichi husaidia kurekebisha kiwango cha sukari na kupunguza hatari ya kuugua kisukari,” Akech ameeleza.

Kwa afya ya nywele na ngozi:

Mafuta yaliyoko kwenye parachichi yanasaidia kuongeza ubora wa ngozi na nywele. Mafuta yajulikanayo kama ‘Omega 9 Fat’ yaliyoko kwenye parachichi yanafahamika zaidi kwa kupunguza wekundu wa nywele na inasaidia kurekebisha seli za ngozi.

Kwa mujibu wa Akech, Vitamin C inayopatikana kwenye parachichi inasaidia pia kutengeneza ‘elastin na collagen’ ambayo hutengeneza ubora na uimara wa ngozi. Ameongeza kuwa Vitamin E pia husaidia afya ya nywele kwa namna nyingi zaidi.

Video: Kopafasta yazinduliwa rasmi nchini
Adukua mtandao wa Serikali na kujiajiri, ajilipa millioni 1.2

Comments

comments