Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Scotland na klabu ya Rangers, Alex McLeish amefikia makubaliano ya kufundisha klabu ya Zamalek ya Misri.

Taarifa ya Zamalek jana iliyoifikia imesema kwamba McLeish, ambaye pia amezifundisha Birmingham City, Aston Villa na Nottingham Forest za England, anachukua nafasi ya Ahmed Hassan ‘Mido’ aliyefukuzwa.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Misri na klabu ya Tottenham ya England alifukuzwa Zamalek wiki mbili zilizopita baada ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa Jiji la Cairo, Al Ahly katika mchezo wa Ligi Kuu.

“Tumefikia makubaliano na kocha Mscotland Alex McLeish kuiongoza timu ya kwanza,”amesema Rais wa Zamalek, Mortada Mansour.

Mansour amesema kwamba McLeish atawasili Misri mara moja kusaini Mkataba na kuanza kazi.

Vinara wa Ligi ya Misri, Al Ahly wanaweza pia kubadili kocha wakati wowote, baada ya magazeti nchini humo kuripoti kwamba wapo kwenye mazungumzo na Martin Jol.

TANZIA: Kassim Mapili Afariki Dunia
Raisi Wa TOC Awataka ZFA Watengeneze Katiba Iliyo Bora