Asasi za Kiraia nchini jana ziliazimia kuanzisha mchakato wa kudai katika mpya huku zikiahidi kutowahusisha wanasiasa katika harakati hizo, tofauti na ilivyokuwa awali.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wao uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Onesmo Ole Nguruma alisema kuwa wameazimia hayo ili mchakato huo uwe wa wananchi na sio wa wanasiasa.

“Mwaka jana mchakato ulikuwa wa kisiasa zaidi, sasa hivi tunataka kuanzisha mchakato utakaokuwa wa wananchi,” alisema Ole Nguruma.

Alisema kuwa baadhi ya wanasiasa walichangia kukwamishwa kwa mchakato huo kwakuwa baadhi yao mwishoni walijikuta wakitofautiana na wengine kuzila kuendelea na harakati hizo.

Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli jana aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari katika mahojiano ya ana kwa ana Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alipoulizwa kuhusu mpango wa kuanzisha upya mchakato wa Katiba Mpya alisema “niacheni ninyooshe nchi kwanza.”

Rais Magufuli alisema kuwa yeye hakulizungumzia suala hilo kwenye kampeni zake zote.

Mchakato wa kupata katiba mpya ulianzishwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete na kuunda Tume iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba ambaye alitengeneza rasimu iliyowagawanya wabunge wa bunge la katiba, wanaharakati pamoja na Serikali.

Wanaharakati wanadai rasimu ya Jaji Warioba iliyowasilishwa kwenye Bunge la Katiba na mapendekezo ya wananchi ndiyo ipewe kipaumbele, huku Serikali ikiwa imebadili baadhi ya maeneo hali iliyoleta mkanganyiko wa mawazo.

 

Lissu aanzisha mgomo nje ya mahakama, adai hana barua
Ndalichako atoa matumaini mapya kwa wanafunzi kuhusu Mkopo