Serikali imesema asilimia 90 ya maoni yaliyotolewa na wadau wa sekta ya habari nchini yanayohusu Muswada wa Huduma ya Habari wa mwaka 2016 yamechukuliwa na kujumuishwa kwenye muswada huo.

Hayo yamesemwa  na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa serikali, Hassan Abbas na kuongezea kuwa moja kati ya jambo la msingi ambalo serikali iliyafanya wakati wa uandaaji wa muswada huo ni kuwakutanisha na kuwashirikisha wadau wa sekta ya habari kutoa maoni ili kuuboresha na kwa kuzingatia umuhimu ya maoni waliyoyatoa kwa kiasi kikubwa serikali imeyajumuisha kwenye muswada huo.

Mkurugenzi Abbas amesema kuwa sekta ya habari ni sawa na sekta nyingine yeyote nchini, ina haki na wajibu wake na kuwashauri wadau kuangalia zaidi  upande wa haki zao zitakazopatikana kwenye muswada huo badala ya kulalamika ili kwa pamoja waweze kulivusha suala hili kwa ustawi wa sekta ya habari nchini.

Aidha, amewataka wadau wa sekta ya habari nchini kuendelea kujenga hoja hasa kwenye maeneo wanayotaka kuboreshwa kwenye muswada huu ili kuisaidia taaluma ya habari kukua na kuheshimika kama fani nyingine nchini na kuiwezesha sekta hiyo iwe rasmi.

Yanga Yaboresha Safu Ya Utendaji
Tofauti ya idadi ya wapiga kura yamtesa Bulaya Mahakamani