Muungano wa nchi za Afrika (AU) umetangaza kuwa hautamtambua Yahya Jammeh kama Rais wa Gambia kuanzia tarehe 19 Januari wakati muda wake utakapokamilika.

Tamko hilo limetolewa na AU kufuatia Rais Jammeh kukakataa matokeo aliyoyakubali hapo mwanzo na ambayo yalimpa ushindi mgombea wa upinzani, Adama Barrow.

Jammeh aliyeliongoza taifa hilo tangu alipochukua madaraka kwa njia ya mapinduzi mnamo mwaka 1994, anasema kwamba kulikuweko na hitilafu katika uchaguzi huo wa Desemba 1, hivyo ametangaza kuwa matokeo ya uchaguzi huo si halali.

Baraza la amani na usalama la AU limesema litachukua hatua kali iwapo vitendo vya Jammeh vitasababisha mauaji ya raia wasio na hatia.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari yuko nchini Gambia akiongoza ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) katika jaribio la kumshawishi Jammeh kuwachilia madaraka kwa Rais mteule, Adama Barrow ambaye alishinda uchaguzi wa Urais mwezi uliopita.

Viongozi wa ECOWAS wamelaani ugeugeu wa Rais Jammeh na kumtaka aachie ngazi, pia wametaka usalama wa rais mteule upewe kipaumbele.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Liberia, Marjon Kamara, amesema viongozi wa ECOWAS wanamtaka Rais Jammeh akubali matokeo na ajiepushe na vitendo vyovyote vitakavyovuruga amani katika makabidhiano ya madaraka kwa rais mteule. “Uamuzi wa Wagambia katika matokeo ya uchaguzi wa Desemba 1 lazima uheshimiwe”, wamesema viongozi hao.

Barrow amesema kwamba Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria na John Dramani Mahama wa Ghana wataendelea kuongoza mazungumzo ya amani na maridhiano.

Rais Jammeh anatarajiwa kukamilisha hatamu za uongozi mwezi Januari, baada ya kuwa madarakani kwa miaka 22.

Msemaji wa upande wa upinzani, Halifa Sallah, alisema iwapo Rais Jammeh ataamua kuendelea kung’ang’ania kubaki madarakani, basi hatua hiyo itamfanya kuwa kiongozi muasi.

“Rais yeyote atakayepoteza haki ya kuliongoza taifa kikatiba moja kwa moja anakuwa muasi ni sawa na mfanyakazi wa serikali au afisa wa jeshi anayekataa kuhudumu chini ya uongozi uliochaguliwa kwa kufuata misingi ya katiba ya nchi, naye vile vile anakuwa muasi.” Amesema Sallah.

Viongozi wa ECOWAS wamesema watahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Barrow kama rais mpya wa Gambia zitakazofanyika tarehe 19 Januari.

#HapoKale
Serikali yazidi kupigilia msumari wa moto shule binafsi