Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amezungumzia mvutano kati ya chama chake na Serikali kuhusu katazo la kufanya mikutano na maandamano ya kisiasa nchini, akieleza kuwa hawana lengo la kumjaribu Rais John Magufuli.

Hivi karibuni, Rais Magufuli aliwatahadharisha kutojaribu kufanya maandamano kama walivyopanga akiwataka wasithubutu kumjaribu kwani yeye ni ‘wa tofauti na hajaribiki’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Lissu ameeleza kuwa chama hicho hakina nia ya kumjaribu Rais wala kuvutana na vyombo vya dola, bali wanachofanya ni kudai haki yao ya kikatiba kwa njia iliyoidhinishwa kikatiba.

“Hakuna mtu anataka haya ambayo tunafanyiwa, hakuna anayetaka kukamatwa… hakuna,” alisema Lissu. “Mahabusu sio pazuri, niwaambie mimi ambaye nimekuwa mgeni wa dola mara mbili katika mwezi uliopita,” aliongeza.

“Lakini tunachotaka kufanya ni kile ambacho Katiba hii inasema tuna haki ya kufanya. Haki ya kukutana na watanzania wengine tuzungumze siasa. Tunataka tufanye kile ambacho sheria ya vyama vya siasa na kanuni yake vinaturuhusu kufanya. Mikutano hadhara ya kisiasa na maandamano halali ya ya kisiasa ya kupinga jambo lolote ambalo linafanywa na mtukufu Rais,” aliongeza.

Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, aliwasihi washauri wa Rais Magufuli kufanya kazi yao ipasavyo kwa kumshauri kuhusu matakwa ya sheria.

Hivi karibuni, Lissu alilala rumande za polisi jijini Dar es Salaam baada ya kukamatwa Mkoani Singida na kusafirishwa hadi jijini humo kwa tuhuma za uchochezi. Hata hivyo, mahakama ilimruhusu kupewa dhamana ya shilingi milioni 10 baada ya mvutano mrefu na mawakili wa Serikali.

Msikilize hapa kwa urefu:

Hatua ya Kwanza Ya Usajili Azam FC wakamilika
Rasmi - John Stones Asajiliwa Etihad Stadium