Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na kuahidi kuendeleza juhudi za jukwaa hilo ili kufikia malengo ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Balozi Mulamula ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji lililofanyika Zanzibar na Dar es Salaam kati ya Tanzania na Italia likiwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka pande zote wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia.

Amesema, “Nawapongeza waandaji wa Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu na sitalifunga bali nitaliahirisha ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia kwani mafanikio yake ni wazi yatasaidia kukuza na kutekeleza Demokrasia.”

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo alitoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini Italia, ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi, huku Balozi wa Italia chini akisisitiza kuimarisha ushirikiano, kupitia majukwaa.

Viongozi mbalimbali, waliohudhuria jukwa hilo, wametumia fursa ya kuwahimiza Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya sheria ambayo ipo tayari wazi kwa umma ambapo Serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji.

Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji, kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022, likiwakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.

Wahimizwa ubunifu upatikanaji maji safi na salama
Tanzania kuendeleza maboresho biashara, uwekezaji