Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango yupo nchini Rwanda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kigali.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo wa siku tano ulioanza Jumatatu ya wiki hii na ukitarajia kuhitimishwa rasmi Juni 25, 2022.

Mbali ya kushiriki kwenye mkutano huo, Mpango atafanya mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Namibia, Hage Geingob, Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Jugnauth, Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau na Melinda Gates.

Mazungumzo hayo ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania Duniani, huku aakitarajiwa kutumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili hasa katika eneo la uwekezaji, biashara na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula yupo nchini humo kushiriki Mkutano huo katika ngazi ya Mawaziri, na anatarajia pia kufanya mazungumzo na Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za India, Zambia, Botswana, Eswatini, Singapore na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair Bi. Cherie Blair.

Mikutano ya utangalizi wa mkutano huo, inaendelea ambapo tarehe 20 hadi 23 Juni 2022 ilifanyika mikutano ya jukwaa la vijana, jukwaa la wanawake na jukwaa la biashara, ambapo washiriki walijadili namna bora ya kufanya biashara katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Uviko-19 na athari za vita vya Urusi na Ukraine.

Ujumbe wa Tanzaia katika mkutano huo uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, ambaye alieleza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania za kuboresha mazingira ya biashara na fursa za uwekezaji zinazopatikana.

Tanzania, Qatar kushirikiana Fainali za Kombe la Dunia
Majaliwa ateta na wanaohama kwa hiari Ngorongoro