Serikali imetenga  kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 8.59 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vitongoji ambavyo havina umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro, katika fedha hizo Wilaya ya Same imetengewa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo wakati akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini Fungu la Pili A ngazi ya Mkoa uliofanyika katika kijiji cha Mheza wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro, utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 12.

Aidha, amewakumbusha  viongozi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Kata na Vijiji kutenga maeneo maalum ya uwekezaji wa Viwanda ili yaweze kupelekewa miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini.

“Tumieni umeme kufanya biashara muongeze thamani ya mazao ya kilimo na mifugo kwa kuanzisha viwanda” Amesema Waziri Kalemani.

Katika hatua nyingine Waziri Kalemani amewaagiza wakandarasi wanaojenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupeleka umeme katika maeoneo maalum ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ameishukuru Serikali kwa kupelekewa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini na kuomba maeneo ambayo bado hayajafikishiwa umeme yapatiwe nishati hiyo.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akiwa na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango,wanafunzi pamoja na viongozi wa wilaya ya Same wakikata utepe kuwasha umeme katika Kijiji cha Kifaru wakati wa ziara ya uzinduzi wa Mradi wa umeme wa Ujazilizi Fungu la Pili ngazi ya  Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika wilayani Same.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akipongezwa na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango mara baada ya kuzindua Mradi wa umeme wa Ujazilizi Fungu la Pili A Ngazi ya Mkoa Uliofanyika katika kitongoji cha Mheza.
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa umeme wa Ujazilizi Fungu la Pili A ngazi ya  Mkoa uliofanyika wilayani Same, uliozinduliwa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.

DKT. Zainab Chaula awafunda wakaguzi wa ndani wa wizara na taasisi zake
Mo Dewji: Usajili Simba ni siri