Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kufuata Sheria, Taratibu na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji.

Waziri Biteko ameyasema hayo alipotembelea Mlipuko wa Madini ya dhahabu uliotokea katika Kitongoji cha Nyambogo, Kijiji cha Nyakafuru, Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita baada ya mkazi mmoja wa eneo hilo kuchimba shimo la choo na kukutana na madini ya dhahabu.

Waziri Biteko amesema kila mahali panapochimbwa madini lazima watu wachimbe kwa kufuata utaratibu na Sheria iliyopo ya mchimbaji kuwa na leseni.

Aidha, Waziri Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wanchimbaji wote wa nchi hii wanachangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini ili wanufaike na madini yaliopo nchini.

“Msidanganywe na mtu, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anataka watanzania wachangamkie fursa, Rais anataka watanzania wamilki uchumi wa madini ndiyo maana amesema maeneo yanayo kaliwa na watu bila kuendelezwa tuyafute na tuwape wachimbaji wadogo, Rais wetu anawapenda sana wachimbaji na anatamani watu watoke kwenye wimbi la umasikini,” Amesema Waziri Biteko.

Aidha Waziri Biteko amewataka Wachimbaji wa madini katika eneo hilo wapendane na kuthaminiana ili wachimbe kwa amani ambapo amesema hiyo dhahabu iliyopatikana katika eneo hilo isiwafanye wagombane na badala yake wapendane na kuthaminiana.

“Mmekutana hapa kwenye shughuli ya madini pendaneni na niwaambie wanambongwe neema hii ameileta Mungu hapa kwenu, kuna watu wanatamani wangekuwa hata na shimo moja la dhahabu lakini Mungu hajawapa ila nyinyi hapa mkichimba mnapata dhahabu, pendaneni thaminianeni,” Amesisitiza Waziri Biteko.

Akitoa taarifa ya Mkoa Mpya wa Kimadini wa Mbogwe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo, Mhandisi Joseph Kumburu amesema, Ofisi ya Mbogwe ni moja kati ya Ofisi 28 za Tume ya madini zilizopo Tanzania Bara ambapo inasimamia wilaya ya Mbogwe, Bukombe na Nyanghwale kwa shughuli zote zinazohusiana na madini.

Jacob Zuma aondolewa gerezani
Al-Saad Gaddafi atoka gerezani