WAKATI uongozi wa Yanga umewasilisha ripoti ya tuhuma za rushwa kwenye Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru), Serikali imesisitiza kuwa haitambui mchakato wa uchauguzi unaoendelea ndani ya klabu hiyo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja alisema kuwa BMT haiungi mkono kinachoendelea ndani ya Yanga kwa vile ni kinyume cha Katiba.

“Kinachofanyika Yanga kwa sasa ni uvunjifu wa Katiba, kama Serikali hatuungi mkono, “alisema Kiganja kwa kifupi. Kiganja ambaye wiki iliyopita pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, Aloyce Komba walituhumiwa na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kuwa walihusika katika uvurugaji wa uchaguzi huo.

Komba baada ya tuhuma hizo alitangaza kujiweka kando kushughulikia uchaguzi huo ili kupisha uchunguzi dhidi yake. Komba sasa ameondolewa na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa na Nidhamu ya TFF katika mabadiliko yaliyotangazwa juzi na shirikisho hilo la soka.

Mapema wiki iliyopita akichukua fomu Makao Makuu ya Klabu ya Yanga, Manji alimtuhumu Komba na Kiganja kushirikiana na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo na TFF kumhujumu kwa kupanga njama za kumuengua katika kinyang’anyiro cha uongozi ndani ya Yanga katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Juni 25.

Katika CD ambayo Yanga wameiwasilisha jana Takukuru zinasikika sauti za baadhi ya watu wakipanga kumhujumu Manji kwa kile walichodai kuwa ni kukosa maadili baada ya kukaa madarakani kinyume cha Katiba.

Akizungumzia tuhuma hizo, Kiganja alisema: “Ninafurahi kama Yanga wamepeleka ushahidi wao Takukuru, naamini haki itatendeka, Yanga wajiandae kunilipa fedha nyingi kwa kunichafua, “alisema Kiganja.

Kwa upande wa Komba alipoulizwa kuhusiana na suala hilo la kuondolewa kabisa kwenye Kamati ya Uchaguzi alisema kwa kifupi: “No comment… No comment…No comment, “alisisitiza.

Hata hivyo alisema kuhusu tuhuma zinazomkabili zilizoelekezwa kwake na Manji, ni kwamba amewasiliana na wanasheria wake ambao wanalichunguza tukio hilo na hatua zaidi zitafuata na kutaka Takukuru kuharakisha suala hili ili haki itendeke kwa pande zote mbili.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga kupitia kwa Ofisa Habari wake, Jerry Muro jana saa sita mchana waliwasilisha ripoti na ushahidi wao wa CD kwenye taasisi ya Takukuru ili iweze kuchunguza tuhuma, ambazo zinawakabili baadhi ya wanachama, watendaji wa TFF na wale wa BMT kumhujumu Mwenyekiti wao Yusufu Manji.

“Tumeamua kuleta suala hili ili kulinda heshima ya klabu yetu na kukomesha figisufigisu, ambazo amekuwa akifanyiwa mwenyekiti wetu, “alisema Muro. Naye msemaji wa Takukuru Musa Misalaba alisema wameshapokea ushahidi huo na wanaufanyia kazi na muda ukifika watatoa maelezo.

Video: Serikali yatangaza TTCL kufanya mambo makubwa kuanzia mwezi Septemba
Jurgen Klopp Kumtema Christian Benteke, Kumsajili Gonzalo Higuain