Botswana imewapa hifadhi wanasoka 10 wa timu ya taifa ya Eritrea waliokataa kurejea nyumbani baada ya kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia, wakili wao amesema.

Dick Barford amesema amejulishwa uamuzi huo na waziri wa haki, ulinzi na usalama wa Botswana Augustine Makgonatsotlhe.

Wachezaji hao walichezea timu yao ya taifa dhidi ya Botswana Oktoba 13, mechi ambayo walishindwa 3-1.

Wengi wa wachezaji soka wa Eritrea wamekuwa wakikataa kurejea nyumbani na kuomba hifadhi baada ya kucheza mechi ugenini.

Wachezaji sita waliomba hifadhi Angola mwaka 2007, 12 nchini Kenya mwaka 2009 na wengine 18 nchini Uganda mwaka 2012.

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloangazia haki za kibinadamu mwezi Juni liliituhumu serikali ya Eritrea kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mamia ya maelfu ya raia wa Eritrea wamekuwa wakitoroka taifa hilo.

Eritrea imekanusha madai ya kukiuka haki za kibinadamu na kusema wanaoondoka nchini humo ni “wahamiaji wa kiuchumi”.

Yanaisha Tanzania, Sasa Ni Zamu Ya FIFA
Baadhi Ya Wajumbe wa ZEC Watofautiana Na Uamuzi wa Mwenyekiti