Beki na nahodha msaidizi wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher anaamini mshambuliaji wa RB Leipzig Timo Werner, anayehusishwa na mpango wa kutua Chelsea kwa ada ya Pauni 54 milioni ilikuwa atue Liverpool kabla ya kuibuka kwa janga la corona.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ujerumani alikuwa anatua Anfield hadi hapo lilipoibuka janga la Corona na kumfanya kocha Jurgen Klopp kuwa na uhakika wa kuwa na mafowadi wake wote watatu, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane kwa muda wote msimu ujao.

Mtazamo wa Carragher ni kwamba dili la straika huyo wa Kijerumani kwenda Liverpool limekwama si kwa sababu ya pesa, bali kwa mambo mengine kabisa.

Wakati michuano ya AFCON ya Januari mwakani ikitarajia kuiga kilichotokea kwenye michuano ya Euro, Olimpiki na Copa America kwa kuahirishwa, jambo hilo linamfanya mshambuliaji Werner kuwa na uhakika hafifu wa kupata nafasi ya kucheza kwenye Ligi Kuu England kama akitua Liverpool, kwa sababu mafowadi wake wote watakuwepo msimu ujao.

Carragher anaamini jambo hilo ndilo lililompa nafasi kocha wa Chelsea, Frank Lampard kwenda kuinasa saini ya Werner kirahisi kwa sababu anafahamu atapata muda mzuri wa kucheza Stamford Bridge kuliko akitua Anfield.

Beki Carragher, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka kwenye televisheni ya Sky Sports alisema safu yao ya ushambuliaji inayoundwa na Mo Salah, Firmino na Mane itakuwa fiti kukipiga huko Anfield na hapo Werner hawezi kupata namba, watakuwa wakali msimu ujao.

Carragher alisema: “Binafsi naamini, kama janga la corona lisingetokea Timo Werner angekuja kuwa mchezaji wa Liverpool.

“Sidhani hili limeshindikana kwa sababu ya pesa. Limeshindikana kwa sababu hakutakuwa na Olimpiki, Afcon na Copa America.

“Kutokana na hilo, kama Werner angesajiliwa na Liverpool, asingepata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu wale washambuliaji watatu wote watakuwepo.

“Angekuja kuwa mchezaji wa kuanzia benchi. Hata hivyo, nadhani Liverpool inahitaji mchezaji wa kiwango cha juu kutokea kwenye benchi licha ya kwamba Divock Origi amekuwa na msaada mkubwa kwa kufunga mabao yake muhimu.

“Lakini, kutumia Pauni 50 milioni kwa mchezaji ambaye unafahamu wazi hawezi kuwa chaguo lako la kwanza ni wendawazimu.

“Kama kungekwua na mashindano ya Olimpiki na Afcon mwakani, Klopp angekuwa na uhakika wa kumhakikishia Werner nafasi ya kucheza mechi za kutosha kwa sababu Salah na Mane wangekosekana.

“Angeweza kucheza mechi 25 hadi 30, lakini kutokana na mashindano hayo kuahirishwa, hapo imekuwa ngumu Werner kusajiliwa, kwa sababu wale fowadi watatu waliopo Anfield, hawakosi mechi.”

Mo Salah, Firmino na Mane wametengeneza kombinesheni matata kabisa katika fowadi ya Liverpool chini ya kocha Klopp.

Kutokana na umuhimu wao kwenye kikosi hicho na kwenye timu zao za taifa, washambuliaji hao wamekuwa hawapewi kabisa muda wa kupumzika, hivyo kipindi hiki cha ligi na michuano mingine kusimama kutokana na janga la corona, ulikuwa wakati wao mzuri kupumzika.

Kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana, Mane alipewa siku 10 tu za mapumziko.

Na katika msimu huo, Klopp bila ya shaka atahitaji huduma za washambuliaji hao muda wote kwa sababu Liverpool itakuwa kwenye mchakamchaka wa kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu England wanaoutarajia kuubeba msimu huu.

Liverpool inahitaji pointi sita tu kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu England, likiwa taji lao la kwanza baada ya kutoka patupu kwa miaka 30.

Carragher amewaambia Liverpool wasahau kuhusu kuvunja rekodi ya pointi 100 za Manchester City na badala yake, ipumzishe wachezaji wake muhimu itakapokamilisha kunyakua ubingwa wa msimu huu, ili wajipange kubeba tena msimu ujao.

“Nafahamu Klopp atataka kubeba ubingwa pia msimu ujao. Kushinda ubingwa msimu huu ni muhimu, lakini kujaribu kushinda tena msimu ujao ni muhimu zaidi,” alisema.

Polisi aliyemuua Mmarekani mweusi kwa risasi kushtakiwa
Ndugai amtaja Bernard Morrison Bungeni