SIKU kadhaa baada ya Serikali kukishinda Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Chadema), katika shauri na. 52/2016 kuhusu uhalali wa tamko la Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara, undani wa kesi hiyo umebainika.

Kwa mujibu wa hukumu iliyopatikana mwishoni mwa wiki, kufuatia kesi ya kuomba mapitio iliyowasilishwa Mahakama Kuu ya Tanzania na Wadhamini wa Chadema, mawakili wa chama hicho cha upinzani wakiongozwa na Peter Kibatala wameshindwa kesi hiyo kwa hoja kubwa mbili za kisheria, uchambuzi wa kina wa hukumu unaonesha.

Katika kesi hiyo upande wa mawakili wa Serikali ukiongozwa na Mawakili wa Serikali, Bw. Haruni Matagane,, Daniel Nyakeha na Bi Lilian Machange ndio uliokuwa mwiba kwa Kibatala.

Akiongoza jopo la mawakili wenzake wa Serikali, Wakili Matagane waliwasilisha hoja kuu mbili Mahakamani kupinga ombi la Chadema kutaka Mahakama ipitie upya na kufuta amri ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano yasiyo na kibali.

Akitoa hoja ya kwanza kupinga ombi hilo, Wakili Matagane, alijenga hoja kuwa ombi la Chadema limewasilishwa kwa namna ambayo imeshindwa kutumia  njia sahihi za  kupinga amri hiyo  kama zilivyoainishwa kwa mujibu wa kifungu cha 43(6)  cha Sheria ya Jeshi la Polisi (The Police Force and Auxilliary Services Act).

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Sheria ya Jeshi la Polisi inaanisha wazi kuwa kabla ya kupinga amri ya polisi ya kuzuia mikutano au maandamano ni lazima kwanza mhusika awasilishe rufaa yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani suala ambalo mawakili wa Chadema hawakuwa wamelifanya

Katika hoja ya pili mawakili wa Serikali pia walitumia kanuni ziitwazo “The Law Reform (Fatal Accidents and Miscellaneous Provisions (Judicial Review Procedures and Fees) Rules, 2014” zinazoainisha kuwa ombi la mapitio lazima liwasilishwe likiwa na kiapo kinachojulikana kisheria kama “statement.”

Mawakili wa Chadema waliwasilisha kiapo hicho lakini kikiwa batili kufuatia kusainiwa au kikionekana kuwa ni kiapo kilichowasilishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) badala ya Wadhamini wa Chadema waliofungua kesi hiyo.

Juhudi za Wakili Kibatala kujibu hoja hizo hazikufua dafu baada ya Jaji Kiongozi, Fernandi Wambali aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, kukubaliana na mawakili wa Serikali kuwa katika kufikisha ombi hilo Mahakamani, Chadema hawakutumia njia ya kwanza iliyoelekezwa na sheria ya kukata rufaa kwa Waziri na pili waliwasilisha kiapo batili.

Kutokana na Mahakama kukubaliana na hoja za Serikali, Chadema pia kimepata pigo jingine ambapo watalazimika kulipa gharama zote za kesi hiyo ikiwa ni fidia kwa Serikali. 

Jeshi la Polisi lilipiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa Julai 7 mwaka huu kupitia taarifa yake iliyotolewa na Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Massanzya ambapo alieleza kuwa Jeshi hilo limechukua hatua hiyo ili kuimarisha usalama wa nchi.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama, amri hiyo ya Polisi inabaki pale pale ikimaanisha kuwa maandamano ambayo Chadema imekuwa ikiyatangaza kuyafanya yanabaki kuwa batili na kwamba vyama vya siasa sasa vitaendelea tu kufanya mikutano yao baada ya kutumia taratibu za kawaida za kuomba kwanza kibali polisi.

Wafilipino Wakataa Rais Wa Zamani Wa Nchi Hiyo Kuzikwa Katika Makaburi Ya Mashujaa Kwa Tuhuma Za Ufisadi
Ziara Ya Jaffo Manispaa Ya Mpanda Yamuweka Matatani Afisa Mipango Miji