Mzimu wa usaliti wa baadhi ya viongozi uliokuwa unakiandama Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa umebainika kukitafuna pia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kimeanza kuwafyeka.

Chadema wameanza kufanya uchunguzi wa kina na kuwabaini viongozi wake mbalimbali waliokisaliti katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Oparesheni hiyo imewavyeka waliokuwa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho wilayani Kyela mkoani Mbeya.

Mratibu wa Chadema Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe amethibitisha kuwa chama hicho kimewavua uongozi aliyekuwa Mwenyekiti wa ngazi ya wilaya (Mbeya Mjini) Saadati Mwambungu na wajumbe 19 wa kamati ya utendaji wa wilaya hiyo baada ya kubainika kuwa walikihujumu chama.

Mwaisumbe alisema kuwa viongozi hao walikuwa na jumla ya tuhuma 17 lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi walibainika kuwa walihusika katika tuhuma 9.

Kati ya makosa yaliyowatimua ni pamoja na matumizi mabaya ya mali na fedha za chama pamoja na kukihujumu chama. Imeelezwa kuwa viongozi hao walichangia katika kushindwa kwa chama hicho jimboni humo kwani katika siku ya kufanya majumuisho ya kura zote walitokomea kabla ya zoezi kuisha.

Kadhalika, wanatuhumiwa kuwasusa vijana wa Chadema waliokamatwa na jeshi la polisi katika vuguvugu la uchaguzi.

“Siku ile ya uchaguzi, kuna vijana wetu walikamatwa wakituhumiwa kuvunja ofisi pale Halmashauri ya Kyela na wakahukumiwa, lakini hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya wilaya aliyethubutu kwenda kuwaona hadi walipojinasua wenyewe,” alisema Mwaisumbe.

Alisema kuwa madaraka yao yamerudishwa kwa uongozi wa Mkoa hadi baada ya siku 30 ambapo uchaguzi utafanyika ili kuwapata viongozi wapya wa ngazi hiyo ya wilaya.

Serikali yagawa Sukari Buree!
Riyad Mahrez Akata Mzizi Wa Fitna, Asema Kinachofuata