Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) chini ya rais wake, Chaulembo Palasa imemfungia kwa miaka miwili bondia Francis Cheka ‘SMG’ kushiriki mchezo huo pia imempiga faini ya Sh 500,000.

TPBC imemfungia Cheka baada ya kugomea pambano lake dhidi ya Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ ambalo lilipangwa kufanyika Desemba 25, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam.

Kutokana na kugomea pambano hilo, Promota Kaike Siraji alimfikisha polisi bondia huyo akitaka amlipe fidia ya Sh milioni 28 ili kulipia gharama alizoingia.

Katibu Msaidizi wa TPBC, Michael Chatta amesema kamati ya utendaji iliyokaa Desemba 27, mwaka huu imeamua kumfungia Cheka baada ya kukutwa na makosa ya kimakubaliano na promota wake.

Chatta alisema kamisheni hiyo ilipokea mkataba wa promota Kaike ukimhusisha Cheka kwa ajili ya pambano lake dhidi Dullah Mbabe huku kukiwa na makubaliano ya kimkataba  kwamba anatakiwa kulipwa Sh milioni tatu za awali na Sh milioni sita baada ya pambano hilo lakini hata hivyo bondia huyo aligomea.

“Kamisheni tumeamua kuchukua hatua ya kumfungia Cheka baada ya kujiridhisha kwamba amechukua fedha pasipo kuifanya kazi aliyotakiwa kuifanya, kitu ambacho hakiwezi kukubalika.

“Kitendo hicho kinapoteza uaminifu, kuwakimbiza wadhamini pamoja na kuleta uvunjifu wa amani. Lakini kwa mujibu wa sheria ya ngumi za kulipwa Tanzania kupitia kifungu cha nne, kifungu kidogo cha kwanza, Cheka amekutwa na mako    sa, hivyo amefungiwa kushiriki kwa namna yoyote mchezo wa ngumi kwa muda wa miaka miwili pamoja na kulipa faini ya Sh laki tano,” alisema Chatta.

Alipotafutwa Cheka na kutakiwa kuizungumzia adhabu hiyo, alisema: “Hao wananifungia kwa lipi? Mimi siyo mwanachama wao halafu nimeshastaafu, sasa hii inatoka wapi, wanajua kwa nini nilikataa kucheza pambano lile?”

Gonzalo Higuain Achizika Kwa Paulo Dybala
Young Africans Wagoma Kusafiri Na Simba SC