Mgogoro wa CUF unaendelea kuchukua sura mpya, baada ya upande wa Mwenyekiti anayetambulia na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Profesa Ibrahim Lipumba, kutoa kauli ikionyesha hofu ya usalama wao na Ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF Masoud Mhina, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni Jijini Dar es salaam,amesema kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Julius Mtatiro, na wenzake wamepanga kuvamia ofisi za chama hicho.
“Tuna taarifa kuwa kuna vijana wanaandaliwa kuja kuvamia Ofisi Kuu za Chama Buguruni kwa ajili ya kufanya vurugu, nadhani wanatufahamu vizuri, tukianza huwa hatukamatiki na tutahakikisha chama kinabaki salama,” amesema Mhina.
Mhina amedai kuwa wanawafahamu viongozi waliopanga hujuma hizo na tayari wamewasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu vitisho na vitendo vya udhalimu vinavyokusudiwa kufanywa na aliowaita wasaliti wa chama hicho, dhidi ya viongozi wa chama upande wa Bara.
Kwa Upande wake Julius Mtatiro amehoji kuwa tangu lini Mwenyekiti wa Chama akachaguliwa na Msajili na kuongeza kuwa Buguruni pamejaa wahuni wanaomlinda Lipumba, hivyo hawawezi kufika eneo hilo.
“Hatuwezi kufanya upuuzi kama huo wa kwenda pale na hakuna anayetaka kuvamia, kwa kuwa hakuna anayetaka kukaa kwenye ofisi ile kimabavu kama Lipumba, tena kwa msaada wa wahuni na Polisi, sasa tunakwenda kuhujumu nini na ili iweje,”amesema Mtatiro.
.
Hata hivyo Mtatiro amesema kuwa ili mtu awe Mkurugenzi lazima ateuliwe na Mwenyekiti halali wa chama anayetambuliwa na vikao vya kitaifa hivyo haelewi wameteuliwa na nani.

Mwigulu: Ruksa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutembea na ving'ora
Serikali kutumia bilioni 105 kutunza nyayo za binadamu wa kale