Wakati serikali ya awamu ya Tano ikiahidi elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka sekondari, wilaya ya Kinondoni imefanya uchunguzi na kubaini udanganyifu mkubwa uliofanywa na wakuu wa shule 68 za msingi na 22 za sekondari.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Salum Hapi  aliagiza uchunguzi ufanyike kuhusu utekelezaji agizo la Rais John Magufuli alilotoa kwa wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua kali walimu wakuu na watendaji wote ambao watafanya udanganyifu na ubadhirifu wa fedha za elimu bure.

Hapi amebainisha hayo mapema hii leo ofisini kwake alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, kuwa wanafunzi 3,462 wa shule za msingi na 2,534 wa sekondari wemebainika kuwa ni hewa na fedha zao hazikupaswa kupelekwa.

“Baada ya agizo la Mh. Rais la kusimamia elimu bure ambalo amekua akitoa kwetu sisi wasaidizi wake, tuliamua kufanya uhakiki wa wanafunzi wetu darasa kwa darasa, Tumebaini udanganyifu mkubwa na tayari nimemuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni awavue madaraka walimu wakuu 68 wa msingi na 22 wa sekondari”alisema Mh.Hapi

Aidha Mh.Hapi alitoa rai kwa watendaji wengine wa wilaya ya Kinondoni wasio waaminifu na wazalendo na wasiofuata sheria na taratibu, kuwa popote walipo atawasaka na watakwenda na maji wasipojirekebisha na kuendana na kasi ya Rais”

Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli alitoa maagizo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi nchini kufuatilia kwa makini fedha za elimu bure ili kubaini udanganyifu na wizi unaofanywa na watendaji wasio waadilifu.

Orijino Komedi wakamatwa, wakutwa na vifaa vya Jeshi la Polisi
Waziri Wa Elimu Prof.Ndalichako Atoa Siku Saba Kwa Vyuo Vikuu Kurejesha Fedha Za Wanafunzi Hewa