Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amesema ujenzi wa majengo mapya ya Chuo cha  Ualimu Kabanga ni moja ya mikakati ya Serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu ya Nchini.

Ameyasema hayo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati wa kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa  majengo mapya ya Chuo hicho ambapo amewataka walimu tarajali kusoma kwa bidii kwa kuwa sasa miundombinu imeboreshwa.

Amesema ni vizuri chuo hicho kikachukua tahadhari zote za kuzuia majanga yakiwemo ya moto na kuwataka  walimu wa Chuo cha Ualimu Kabanga watakaohamia katika majengo mapya ya Chuo hicho  kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

“Serikali ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan inathamini urafiki  wa muda mrefu na ndugu zetu wa Canada, nakuomba Balozi kupitia kwako utupelekee salamu zetu  kwa Waziri Mkuu wa Canada kutoka kwa Watanzania, tunaishukuru serikali yake pamoja na wananchi kwa kuendelea kushirikiana nasi  tunapofanya jitihada za kujikomboa kielimu na  katika maeneo mengine ya nchi yetu  Canada imekuwa mbia muhimu,” amesema Makamu wa Rais

Naye Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako amesema Mradi  huo mpaka utakapokamilika utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 11 na kwamba umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Programu ya Kuimarisha Elimu ya Ualimu (TESP).

Naye balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O’donnel amesema Canada inayofuraha kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika juhudi za kuboresha mfumo wa ufundishaji kwa faida ya watoto wa kitanzania.

Tuchukue tahadhari tusije tukaangamia
Mosimane afunguka silaha iliyowaua Kaizer Chiefs