Doria ya Askari wa Wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatarajiwa kuanza leo ili kufukuza tembo waliovamia kijiji cha Mbute na Ngulichile Wilayani Nachingwea .

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza changamoto za wananchi iliyofanyika leo Wilayani Nachingwea.

“Ninawaagiza askari wa wanyamapori kuhakikisha mnaweka kambi katika vijiji hivi na kuanzia leo mfanye doria ya kuangalia tembo walipo ili kuwarudisha katika maeneo yao ya hifadhi” Mhe. Masanja amefafanua.

Amesema doria hizo zitakuwa mwarobaini wa kutatua tatizo la tembo waliovamia makazi ya wananchi katika vijiji hivyo.

“Kambi hii a askari wa wanyamapori katika maeneo haya iwe ya kudumu lakini naelekeza askari waje leo kufukuza tembo ili wananchi waishi kwa amani” amesisitiza mhe. Mary Masanja.

Masanja amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea pamoja na wananchi wa Wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kukamilisha zoezi hilo.

Aidha, Mary Masanja amewaagiza wananchi hao kuanza utamaduni wa kufuga nyuki ili kukabiliana tembo.

“Nawaagiza watakapokuja wakufunzi kutoka Wizarani kuwafundisha mbinu mbalimbali za kukabiliana na tembo, mkubali njia hii ya kufuga nyuki kwa sababu nyuki ni adui wa tembo, sehemu ambayo nyuki yupo tembo hawezi kukaa”  Mary Masanja ameongeza.

Amefafanua kuwa ufugaji nyuki utasaidia kurutubisha mazao yao korosho wanayolima ili yaweze kukua vizuri.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya tembo, Diwani wa Kata ya Ngulichile, Mhe. Said Mwakayola amesema kuwa wananchi wanaogopa kwenda kwenye maeneo yao ya shughuli za kila siku kama kisimani na mashambani kutokana na tatizo hilo la tembo.

“Zoezi hili la kufukuza tembo naomba lianze haraka iwezekanavyo kwa sababu watu wanashindwa kwenda hata kwenye mashamba ya mikorosho kuangalia mazao yao kwa sababu ya tembo hawa” amefafanua Mwakayola.

Pia, Mwakayola ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa askari wa wanamapori watakaoanza zoezi hilo la kukabiliana na tembo.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi za kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kama tembo wanaovamia makazi ya wananchi katika sehemu mbalimbali nchini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akimsikiliza Mhifadhi wa Makumbusho ya Majimaji na ya Kumbukumbu ya Dkt. Rashid Mfaume Kawawa, Balthazar Nyamusya (kushoto) akitoa maelezo kuhusu handaki lililopo kwenye Makumbusho ya Dkt. Rashid Mfaume Kawawa alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua eneo hilo lililopo Bombambili Wilaya ya Songea .

LHRC yazindua Ripoti ya haki za binadamu na biashara
Ashikiliwa na Polisi kwa madai ya kujiteka ili apate fedha za kulipa madeni