Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng Godfrey Kasekenya amewataka Meneja wa TANROADS mkoa wa Simiyu Eng. John Mkumbo na wa Singida  Eng. Joseph Masige  kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda madaraja na kuhakikisha kingo za daraja hilo zinaimarishwa ili kuliwezesha kukabiliana na changamoto za mafuriko wakati wa mvua kubwa.

Ameyasema hayo wakati akikagua daraja la Msingi lililopo wilayani Mkalama mkoani Singida, ambapo Naibu Waziri Kasekenya ameridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea wa daraja hilo.

Daraja hilo ni miongoni mwa madaraja makubwa yaliopangwa kujengwa tangu wakati wa uhuru hivyo kukamilika kwake kutaleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa mikoa ya Singida, Simiyu na Manyara.

“Tunapoadhimisha miaka sitini ya uhuru wa Tanzania Bara ni fahari kubwa kuona daraja hili ambalo ujenzi wake ulikuwa ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sasa umefikia asilimia 75 kukamilika”, Amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Singida Eng. Joseph Masige  amesema daraja hilo lenye urefu wa mita 100 na upana wa mita 10 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa KM 1 linajengwa na mkandarasi  mzawa GEMEN ENGINEERING CO. LTD kwa gharama ya shilingi bilioni 10.9 na linatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwakani.

Katika hatua nyingine Eng. Kasekenya amekagua daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82, ambalo ujenzi wake umekamilika na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kulinda miundonmbinu ya daraja hilo ili lidimu kwa muda mrefu.

Daraja la Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida kupitia wilaya za Meatu na Mkalama linaunganisha kwa njia fupi mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa na hivyo litachochea unafuu wa huduma za kijamii na biashara baina ya wakazi wa mikoa hiyo.

Air Bus 220-300 yatua Lubumbashi
Bilioni 5 kujenga kituo cha mafunzo ya upimaji ramani