Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga ameitaka Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo – FADev, kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ili Serikali na jamii itambue kazi zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Mwanga ameyasema hayo hii leo Machi 22, 2023 alipokutana na uongozi wa taasisi ya FADev uliofika kwa lengo la kujitambulisha na kueleza majukumu yanayofanywa na taasisi hiyo kuendeleza uchimbaji mdogo katika kikao kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba, jijini Dodoma.

Amesema, FADev inatakiwa kushirikiana na Serikali ili kujenga mahusiano mazuri katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na kusaidia kuepusha kuingiliana na majukumu hayo mara kwa mara na kuitaka kuendelea kuilinda taasisi hiyo kwa kuheshimu taratibu na misingi iliyowekwa na nchi, ambayo inalinda utu wa watanzania katika majukumu yao.

Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa FADev, Mhandisi Theonestina Mwasha amesema wanaendelea kutekeleza miradi inayokuza na kuimarisha uzalishaji wa dhahabu na kusema sema, taasisi hiyo imetoa vifaa vya uchimbaji migodi kwa vikundi mbalimbali walivyofanya navyo kazi sambamba na kuimarisha vikundi vya wanawake 15 katika mikoa ya Geita na Shinyanga.

“Tunafanya mafunzo  katika maeneo ya uchimbaji, tunatoa elimu  shirikishi kwa jamii inayozunguka migodi nakuanzisha mchakato wa kutoa elimu ya kuongeza thamani kwa ushirikiano wa wadau,” amesema Mhandisi Mwasha.

Hadi sasa, taasisi ya FADev imefanikiwa kutoa mbinu za ujasiriamali kwenye maeneo ya uchimbaji madini, mafunzo ya utunzaji wa mahesabu, mafunzo ya ukusanyaji na utunzaji wa taarifa na matumizi sahihi ya kemikali zinazotumika kwenye uchenjuaji.

Azam FC yafuta safari ya Nairobi-Kenya
Clatous Chama aiteka tena Afrika