Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Wales Gareth Bale yu mashakani kuukosa mchezo wa ligi ya nchini Hispania ambao utashuhudia Real Madrid wakisafiri kuelekea mjini Barcelona kupambana na FC Barcelona mwanzoni mwa ujao.

Hofu ya mshambuliaji huyo kuukosa mchezo huo maarufu kama El Clasico, imeibuka kufuatia kuumia kifundo cha mguu usiku wa kuamkia hii leo alipokua katika jukumu la kuitetea Real Madrid katika mchezo wa mzunguuko wa tano wa ligi ya mabingwa bingwa barani Ulaya dhidi ya Sporting Lisbon.

Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane alithibitisha taarifa za kuumia kwa Bale mwenye umri wa miaka 27, alipokuzungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo uliounguruma mjini Lisbon nchini Ureno na kuhushudia mabingwa hao watetezi wakiibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

“Ameumia kifundo cha mguu, lakini tunapaswa kusubiri hadi atakapofanyiwa vipimo,” Alisema Gwiji huyo wa soka kutoka nchini Ufaransa.

“Jopo la madaktari wetu litatupa majibu sahihi, na tutafahamu itamchukua muda gani kupona, kwani najua kila mmoja kwa sasa atataka kufahamu kama mchezaji huyu atakuwa na uwezo wa kuuwahi mpambano dhidi ya FC Barcelona.” Aliongeza Zidane

Real Madrid kwa sasa wapo kileleni mwa msimamo wa ligi ya nchini Hispania (La Liga) na wana faida ya point nne dhidi ya mahasimu wao wakubwa FC Barcelona.

Katika mchezo wa jana, mabao ya Real Madrid yalipachikwa kimiani na wachezaji kutoka nchini Ufaransa Raphael Varane na Karim Benzema katika dakika ya 29 na 87 huku bao la kufutia machozi kwa upande wa wenyeji likifungwa na Adrien Silva kwa njia ya mkwaju wa penati dakika kumi kabla ya kupenga cha mwisho kupulizwa.

Video: Polisi - Siasa inatukwamisha, Mawakili kesi ya Lema wakwama
Mzimu Wa Majeraha Wamuandama Vincent Kompany