Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gerson Msigwa amesema, hapendezwi na kinachoendelea kati ya Kiungo kutoka Visiwani Zazibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ na Uongozi wa Young Africans.

Pande hizo mbili zimeingia kwenye mgogoro wa kimkataba tangu mwishoni mwa mwaka 2022, hali iliyopelekea kesi yao kusikilizwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ mara mbili.

Msigwa ameweka wazi kuchukizwa na sakata hilo alipohojiwa na Clouds FM mapema leo Jumatano (Machi 15), huku akiahidi kuzungumza na Rais wa Young Africans Hersi Said endapo atakutana naye, ili kutafuta mbinu mbadala ambazo zitakuwa suluhisho.

“Sisi kama Wanamichezo tungependa kuona hili jambo likifikia mwisho. Sijakutana na Rais wa Young Africans Hersi Said kuzungumza nae suala hili. Feisal haishii tu kuwa mdogo wangu, lakini pia huyu ni mchezaji ninayempenda.”

“Anacheza wapi, hilo ni jambo lake yeye, lakini natamani kumuona akirudi kucheza kwa ajili ya kiwango chake na mchango wake kwa taifa letu.” Amesema Msigwa

Tayari Feisal Salum amewasilisha Barua TFF akitaka Mkataba wake na Young Africans kuvunjwa, baada ya kukwamba mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo imeendelea kumtambua kama mwajiriwa na Young Africans.

Simba wa Serengeti, Bob Junior afariki dunia
Kamishna wa Uhifadhi TAWA ala kiapo cha utumishi