Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri, yaliyolenga katika kuziba pengo lililoachwa na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Taarifa kutoka Ikulu imeeleza kuwa Rais Magufuli amemteua mbunge wa Buchosha, Dk. Charles John Tizeba kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Mwigulu Nchemba.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Charles Kitwanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kubainika kuwa aliingia Bungeni na kujibu swali la wizara yake akiwa amelewa.

“Mawaziri walioteuliwa katika mabadiliko haya wataapishwa Jumatatu, tarehe 13 Juni,2016 saa 3:00 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

 

Basi la Mwendokasi lamuua Mlemavu
Wanafunzi St. Joseph waanza kuitesa TCU, Mahakama kuu yaridhia