Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba hakuna mgonjwa atakayekwenda kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati bila ya kupatiwa dawa.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale Mkoani Lindi katika mkutano wa hadhara.

Amesema kuwa moja kati ya ajenda muhimu ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kila mwezi halmashauri zote nchini zinapelekewa fedha za ununuzi wa dawa.

“Serikali hii ya Rais Dkt. John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa kila mwezi katika halmashauri zote nchini, Sasa kama hapa Liwale kuna malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika hospitali yetu, Mkuu wa Wilaya kafuatilie huko Halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa,”amesema Majaliwa

Aidha, amesema kuwa katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 236 zimetengwa kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

Hata hivyo, kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema kuwa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 iliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015/2016.

 

Video: ukuaji wa uchumi unategemea afya bora za wananchi-Mkapa
Video: Siwezi kustaafu uanachama wa CCM mpaka Mungu anichukue-Mkapa