Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba; “Hakuna raha kubwa duniani kama kumfunga” Yanga SC.

Hans Poppe amesema hayo kuelekea mpambano wa watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba Yanga lazima ‘atafunwe’ Jumamosi kwa sababu kubwa mbili, ambazo amezitaja ni kuwashikisha adabu watani na pia Simba kujiweka vizuri katika mawindo yake ya ubingwa.

“Furaha ya kuwanyoa Yanga ni mara tatu ya furaha ya kawaida, kwani kipigo wanachopata watani wetu hao katika soka ni sherehe tosha kwa Simba, haswa kwa mbwembwe za mashabiki wetu,” amesema Hans Poppe.

Simba SC imeweka kambini mjini Morogoro kujiandaa na mchezo huo, ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo mjini Shinyanga 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na 2-1 dhidi ya Stand United.

Mahasimu wao, Yanga SC wameweka kambi Pemba visiwani Zanzibar, wakitoka pia kushinda mechi mbili mfululizo, 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika Ligi Kuu na 1-0 ugenini dhidi ya Cercle de Joachim nchini Mauritius katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ikumbukwe mchezo wa kwanza mwaka jana, Simba SC ilichapwa 2-0 mabao ya Malimi Busungu na Amissi Tambwe na Jumamosi ijayo watakuwa na deni la kulipa.

TFF Yaipongeza African Lyon
TFF Yasikitishwa Kupigwa Kwa Mwandishi