Mwimbaji na muigizaji maarufu, Hemed ‘Phd’ Suleiman ameeleza jinsi ambavyo matumizi ya dawa za kulevya yaliyomteka baba yake mzazi yalivyoiathiri familia yake. Lakini yeye aliyasoma na kuyatumia kama funzo lililomjenga tofauti katika maisha na jamii iliyokuwa inamzunguka.

Msanii huyo amekiambia kipindi cha Ladha 3600 cha E-Fm kuwa baba yake mzazi alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa kifedha lakini baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya, ndoto za awali alizokuwa nazo msanii huyo wakati huo ziliyeyuka.

“Mimi binafsi ni mmoja kati ya watu ambao baba yangu aliathirika na madawa ya kulevya kwahiyo niliona namna gani yalimtesa kiasi cha kupelekea kuharibu maisha yetu sisi wakati tuko wadogo,” Hemed alisimulia.

“Baba yetu alikuwa ni mtu ambaye alikuwa na uwezo sana kwahiyo sikutegemea kama maisha yangu yangekuwa hivi. Sikutegemea kama ningepita njia ya sanaa mimi kunitoa kimaisha. Nilikuwa nategemea future (maisha ya siku za usoni) nzuri ambayo imeandaliwa na mzazi wangu. Pengine ningekuwa ‘somebody’ huko,” aliongeza.

Alisema kuwa kutokana na athari alizoziona kwa baba yake, hakuwahi hata siku moja kutumia aina yoyote ya dawa za kulevya ingawa aliishi na marafiki wa karibu waliokuwa wanatumia na wakati mwingine yeye kutumika kama daraja ya kuyapitisha.

“Mimi nilishakaa maskani ambayo bangi inatoka upande huu inaenda upande huu na ninaipitisha mimi katikati lakini sijawahi hata siku moja kufikiria hata kujaribu,” alimueleza kwa msisitizo mtangazaji wa Ladha 3600, Jabir Saleh.

“Kutona kwamba mzee aliamua kwenda njia hiyo, funzo likaonekana, madhara yakaonekana, majuto yakaonekana, mwisho wa siku sidhani kama itakuwa ni vyema kupita kule mzee alikopita wakati mimi nilishaona funzo kubwa kutoka kwa mzazi ambaye amenileta duniani,” alisema.

Hemed alianza kuikimbiza ndoto yake mpya rasmi kupitia kipaji chake mwaka 2008 aliposhiriki mashindano ya Tusker Project Fame jijini Nairobi nchini Kenya na kung’aa vilivyo. Wengi walimfananisha na Usher Rymond akiwateka mashabiki hasa wa kike. Mwaka 2011 alirudi katika mashindano hayo tena akiwa ni msanii maarufu kutoka Tanzania akiwa na uwezo mkubwa zaidi.

Hivi sasa ni ‘hitmaker’ asiyezoeleka kwenye RnB na akimmulika na lens ya kamera, kipaji chake cha kuigiza kitakuchukulia muda wa kutosha kuangalia TV yako.

Ushuhuda huo wa Hemed umekuja siku chache baada ya rapa wawili wakubwa nchini, Chid Benz na Young Dee kujitokeza hadharani kukiri kutumia dawa za kulevya na kusaidiwa kurudi kwenye maisha ya kawaida.

‘Taswira ya Ali Kiba ndani ya studio ya Diamond inaongea kitu’
Waziri: Uteuzi uzingatie usawa wa kijinsia