Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal ‘Omdurman’ Florent Ibenge amesema, anaamini Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wana nafasi kubwa ya kufanya maajabu kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Ibenge yupo nchini Tanzania kwa sasa sambamba na kikosi cha Al Hilal, kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya kuelekea mchezo kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kocha huyo kutoka nchini DR Congo amesema: “Ninaamini Young Africans huko walipo kwenye Michuano ya Shirikisho Barani Afrika wanayo nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa kuwa tayari wanao wachezaji wengi sana wenye uwezo mzuri na wenye wazoefu mkubwa katika michuano hii.”

“Yupo Fiston Mayele, Stephene Aziz Ki, Bernard Morrison, Yannick Bangala na Djuma Shabani wote hao ninawafahamu na ni wachezaji wazuri ambao wana uwezo mkubwa sana na naamini wataifikisha mbali sana hiyo timu.”

“Young Africans ukiwatazama wana malengo makubwa kama ambavyo nimekuwa nikiwafahamu siku zote, lakini ambacho wanatakiwa kukifanya kwa sasa ni kuweza kupata matokeo mazuri haswa wanapokuwa nyumbani, hilo jambo la msingi sana kwao, naamini watafanikiwa.”

Ikumbukwe kuwa Ibenge ndiye aliyewaondoa Young Africans akiwa na Al Hilal kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kisha Young Africans ikaangukia kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Waandishi watatu wa TV wafutwa kazi kwa kulikejeli Bunge
REA yaungana na Wadau usimamizi miradi ya Umeme