Israel imeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua tahadhari mapema na kupokea kwa masikitiko taarifa za uchaguzi wa Iran, ambapo Ebrahim Raisi anakuwa Rais mpya wa taifa hilo.

Msemaji wa Wizara ya Nje ya Israel, Lior Haiat amesema Bw. Raisi ni kiongozi mwenye msimamo mkali zaidi na anaweza kuwa na uamuzi wa hatari ikiwa ni pamoja na kuongeza shughuli za uzalishaji wa makombora ya nyuklia. Amesem hatua hiyo itakuwa tishio kwa usalama.

Jana, Ebrahim Raisi alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais katika uchaguzi ambao ulionesha kumpa nafasi yeye zaidi dhidi ya wengine waliokuwa wanawania nafasi hiyo.

Baada ya kutangazwa kuwa kiongozi wa juu zaidi, Bw. Raisi ambaye ataapishwa rasmi Agosti mwaka huu, ameahidi kuunda serikali itakayoaminiwa na umma na kwamba atakuwa kiongozi bora kwa wananchi wote.

“Nitaunda taifa la wachapakazi, taifa la mapinduzi linalopambana na rushwa,” alikaririwa na vyombo vya habari.

Kiongozi huyo alikuwa Jaji wa ngazi ya juu wa Taifa hilo. Ni mmoja kati ya viongozi ambao Marekani na washirika wake imewawekea vikwazo.

Iran na Israel wamekuwa katika mgogoro wa muda mrefu, ambao umekuwa kama vita ya kuviziana na ya kimyakimya. Hata hivyo, nchi hizo zinaonekana kukwepa kuingia kwenye vita ya moja kwa moja, ingawa katika siku za hivi karibuni mvutano kati yao unaongezeka. Israel ikijikita katika kupinga mradi wa nyuklia wa Iran.

Aharibu mazao ya Sh4 Milioni, baada ya mkewe kukataa kupumzika ‘Siku ya Baba Duniani’
Bidhaa zenye thamani ya millioni 200 zakamatwa