Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Arnold Kihaule kwenda mkoani Morogoro leo Novemba 20, 2019 kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Ametoa maagizo hayo alipompigia simu Mkurugunzi Mkuu huyo wa NIDA baada ya kuambiwa na wananchi wa mkoa huo kuwa kero yao ni uhaba wa ofisi za NIDA kwa kulinganisha na mahitaji yao.

“Mbona watu wa Kilosa wanapata shida, nataka watu waliopo wilayani wasihangaike kuja hadi mkoani, uje hapa Morogoro mlifanye hili zoezi haraka kusudi watu wasajili simu zao,”  Rais Magufuli alimuagiza Kihaule kwa njia ya simu.

Mkurugenzi huyo aliyapokea maagizo hayo ya Mkuu wa nchi na kukiri kuwa kuna ofisi mbili tu katika mkoa wa Morogoro ambazo hazitoshi kwa kulinganisha na mahitaji ya wananchi. Alisema ofisi moja iko Tungi na nyingine ipo mjini Morogoro.

Rais Magufuli amemtaka kuhakikisha huduma ya ofisi za NIDA ipo kila wilaya ili kuepusha usumbufu na gharama za usafiri kwa watu wanaohitaji huduma hizo kutoka wilaya tofauti. Amesema kuwa maagizo hayo yanapaswa kufanyiwa kazi nchi nzima.

Rais Magufuli amempa siku tatu Mkurugenzi Mkuu huyo wa NIDA kuhakikisha anatoa ripoti ya namna alivyoyafanyia kazi maagizo yake.

Magufuli "Ukiona mahindi yapo bei juu nenda kalime yako"
Live: Magufuli akitatua kero za Wananchi Kibaigwa mkoani Dodoma