Jukwaa la Katiba Tanzania limerudisha mezani mjadala wa mchakato wa kupata Katiba Mpya nchini huku likiwasilisha ombi  lake kwa Rais John Magufuli.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa wanamuomba Rais Magufuli kujitokeza hadharani na kutangaza tarehe rasmi ya kuendelea na mchakato wa kupata Katiba Mpya.

“Kama sehemu ya kufufua upya mchakato wa Katiba, na njia ya kurudisha hamasa ya wananchi, Jukwaa la Katiba Tanzania linashauri kwamba Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ajitokeze hadharani, alitangazie Taifa tarehe na namna ya kurejea kwenye mchakato na namna ya kukamilisha hatua zilizobaki,” alisema Kibamba.

Kibamba amesema kuwa wameamua kutoa ombi hilo kwa Rais Magufuli wakati huu ambao Watanzania wanaihitaji Katiba Mpya kwakuwa uzoefu wao unaonesha kuwa marais wapya wanaoingia madarakani Barani Afrika huachana na mambo yaliyoachwa na watangulizi wao na badala yake kuanzisha yale wanayoamini yanafaa kupewa kipaumbele katika utawala wao.

Kibamba alisema kuwa Mchakato wa Katiba haukusitishwa na Serikali ya Awamu ya Nne bali ulisimama wenyewe.

“Tunashauri kufanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza na kurejesha Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili iendelee na kumalizia kazi yake,” alisema Mwenyekiti huyo.

Mchakato wa Katiba Mpya uliogharimu Mabilioni ya fedha ulisitishwa mwaka jana kupisha uchaguzi mkuu baada ya Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi yake.

Hata hivyo, Mchakato huo uliibua makundi mawili ambayo yalikuwa yakipingana kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Kati ya Makundi hayo, vyama vya upinzani viliunda kile walichokiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Philip Mangula awajibu wanaodai CCM inahofu kumkabidhi Magufuli uenyekiti
Video: Mataifa 54 kufika Tanzania Kongamano la maji Afrika