Kuanza kurejea kwa Wachezaji waliokua majeruhi katika kikosi cha Simba SC, kumempa faraja Kaimu Kocha Mkuu wa Klabu hiyo Juma Ramadhana Mgunda, ambaye ana kazi ya kurejesha furaha ya Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2022/23.

Mgunda amesema anafurahi kurudi kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu waliokuwa majeruhi akiwamo mchezaji mwandamizi, Shomari Kapombe ambaye alimtumia kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, Jumapili (Oktoba 30).

“Kuhusu hali ya majeruhi ndani ya kikosi, mpaka sasa ni mlinzi wa kulia tu, Israel Mwenda na Jimmyson Mwanuke ndio bado wanaendelea kupata matibabu,” amesema.

Amesema Mwenda anatarajia kurudi uwanjani hivi karibuni kutokana na kuendelea vizuri na matibabu wakato Jimmyson akitarajiwa kuwa nje kwa muda zaidi.

Mgunda amesema anajua mapambano kati yao na watani zao ni makubwa, lakini kitu cha msingi yeye anaangalia zaidi mechi zao kuhakikisha wanacheza vizuri na kupata ushindi mwisho wa msimu ndio atajua timu gani imekuwa bingwa.

Jumapili iliyopita Simba ilitoa dozi nzito ya mabao 5-0 kwa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kipigo ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kutolewa tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Mwezi huu Simba SC inakabiliwa na Michezo sita ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo itaanza kucheza dhidi ya Singida Big Stars katika Uwanja wa Liti mkoani Singida Novemba 9 kabla ya siku tatu baadaye kurejea Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha Ihefu FC.

Novemba 16, Simba itashuka tena katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuialika Namungo FC na siku tatu baadaye itakuwa ugenini kuvaana na Ruvu Shooting kabla ya Novemba 23 kuifuata Mbeya City katika Dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Kwa sasa Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 17 katika michezo nane, wakizidiwa alama tatu na watani wao wa jadi, Young Africans walioko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Mwakalebela apoteza matumaini Kimataifa
Waraabu wa Tunisia wamuibua Hassan Bumbuli