Aliyekua Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Fredick Lameck Mwakalebela ni kama ametakata tamaa kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani, kufuatia sare ya bila kufungana dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Young Africans itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili mjini Tunis-Tunisia Jumatano (Novemba 09), ikiwa na kazi kubwa ya kusaka matokeo ya ushindi ama sare ya mabao yatakayoipeleka Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho.

Mwakalebela amesema anafahamu jukumu ni zito sana kwa Wachezaji na Kocha Nasreddine Nabi watakapokua nchini Tunisia juma lijalo, lakini amewapa moyo wa kupambana.

Hata hivyo Mwakalebela ameutaka Uongozi wa Young Africans kuhamisha nguvu kubwa kwenye Michauno ya ndani (Ligi Kuu Tanzania Bara), ili kuepuka kuutema ubingwa kwa watani zao wa jadi Simba SC.

“Presha ipo kubwa katika timu hivi sasa, hiyo ni baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia Shirikisho, hivyo Kocha, Wachezaji na Viongozi wanatakiwa kujiongeza.”

“Ninafahamu kwamba hivi sasa Young Africans wanatakiwa kuthibitisha ubora wao kwa kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho wakitumia nguvu na akili nyingi.”

“Hawatakiwi kufanya hivyo wakajisahau, badala yake kuipa umuhimu mchezo ya Ligi Kuu, kwa lengo la kutetea ubingwa wetu, kwani Simba SC wanasubiri tuteleze kidogo ili watupokee Ubingwa msimu huu.” amesema Mwakalebela

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 20, tofauti ya alama tatu dhidi ya Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 17 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya tatu, ikizidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Nasreddine Nabi amfagilia Aziz Ki
Juma Mgunda atabasamu Simba SC