Meneja wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameripotiwa kuongoza harakati za kumnasa kiungo mshambuliaji wa Bayer 04 Leverkusen ya Ujerumani, Kai Havertz.

Solskjaer anaamini kiungo huyo atatosha kuleta mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kuanzia msimu ujao, endapo atafanikiwa kumsajili wakati wa dirisha la usajili (Usajili Wa Majira Ya Kiangazi).

Meneja huyo kutoka nchini Norway pia amedhamiria kumsajili kiungo wa  Borussia Dortmund, Jadon Sancho, ambaye mwishoni mwa juma lililopita alipiga hat-trick wakati timu yake ilipoichapa Paderborn 6-1 kwenye ligi ya Bundesliga.

Hata hivyo mpango namba moja wa Solskjaer ni kumsajili Sancho, lakini baada ya hapo atajizatiti kumnasa Havertz, ambaye anaamini asipofanya hivyo kwa mwaka huu, huenda thamani yake ikuwa kubwa zaidi mwakani.

Kwa kuanzia, Man United wamepeleka ofa ya Pauni milioni 50 kwa ajili ya ushawishi wa usajili wa Havertz, huku wakiamini kitita hicho kitatosha kuipata saini ya mchezaji huyo.

Havertz amekuwa akiwindwa na vigogo msimu huu baada ya kufunga mabao 15 katika michuano yote. Man United wameshafahamu watamtumiaje, ikiwa ni pamoja na kumchezesha kwenye wingi moja au akitokea kwenye kiungo ya kati.

Mpango ni kwamba Havertz atacheza kulia, kushoto atakuwapo Sancho na Marcus Rashford atasimama katikati. Hata hivyo, huduma ya Sancho haiwezi kupatikana kirahisi, lazima mkwanja unaoanzia Pauni 100 milioni na kuendelea.

Aidha, Man utd wamekubaliana na klabu ya Shanghai Shenhua ya China kubaki na Odion Ighalo hadi Januari 2021.

20 wakamatwa Katavi kwa ‘kunyofoa’ nyeti za watu
Ibrahim Ajibu alimwa mshahara Simba SC