Dada wa mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, Ruth, ametangazwa mshindi wa wadhifa wa Mwakilishi wa Kike kutoka kaunti ya Kisumu.

Ruth, ambaye aliwania kiti hicho kwa tiketi ya ODM alikuwa akikabiliana na washindani wengine watatu.

Katika matokeo yaliyotangazwa na IEBC, Ruth alipata kura 304,293 dhidi ya Valentine Otieno wa Movement for Democracy and Growth MDG ambaye alimfuata kwa umbali na kura 80,117 na Rose Auma ambaye alikuwa mgombea huru wa kiti hicho alikuwa wa tatu kwa kura 36,692.

Mgombea wa United Democratic Alliance (UDA) Filgona Atieno alikuwa wa nne na kura 7, 825.

Kuanzia mwaka wa 2013 hadi 2017, Ruth alihudumu kama naibu gavana wa aliyekuwa gavana wa kwanza wa Kisumu, Jack Ranguma.

Wadhifa wa Mwakilishi wa Kisumu ulikuwa na ushindani mkali baada ya aliyekalia kiti hicho Rozaah Buyu kuamua kuwania kiti cha ubunge wa Kisumu Magharibi, ambacho alishinda.

Katika Bunge la Kitaifa, Ruth Odinga ataungana na wawakilishi wengine 46 wa kike na wabunge 290 waliochaguliwa.

Wabunge wengine 12 watapendekezwa na vyama vinavyowakilishwa katika Bunge hilo kwa msingi wa uzito, kumalizia muundo wa wanachama 349.

Kenya: Vita ya ubunge yakolea Azimio wakiongoza
Kenya: Ruto 49.91%, Odinga 49.41%