Washitakiwa 24 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Askari Polisi Wilayani Ngorongoro wameachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Arusha, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kusema hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa hii leo Novemba 22, 2022 dhidi ya washitakiwa hao 24, ambao kumi kati yao ni madiwani wakiungana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ngorongoro, Nderango Laizer.

Mahakama imeambiwa kuwa, kwa niaba ya Jamhuri DPP hana nia ya kuendelea kuwashitaki watuhumiwa hao, na kuomba kuondoa shauri hilo mahakamani kupitia kifungu cha 91(1), cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Nderango Laizer (mwenye koti ya bluu), akisalimia na ndugu nje ya Mahakama jijini Arusha baada ya kuachiwa huru.Picha ya Janeth Mushi

Kesi hiyo, ilikuwa ni dhidi ya watuhumiwa Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Moloimet Yohana, Joel Clemes Lessonu Morijoi Parmati, Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Morongeti Meeki na Kambatai Lulu.

Watuhumiwa wengine ni Taleng’o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Simon Orosikiria, Damian Rago Laiza, Joseph Lukumay Mathew Eliakimu, Luka Kursas, James Taki, Simon Saitoti na Wilson Kiling.

Wote kwa pamoja, walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili ya kudaiwa kula njama ya kuua maafisa wa Serikali na maafisa Polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka ya pori tengefu la Loliondo na kosa la pili ni la mauaji ikidaiwa kuwa Juni 10, 2022 kwa nia ovu walisababisha kifo cha G 4200, Koplo Garlus Mwita katika eneo la Ololosokwan lililopo Wilayani Ngorongoro.

Wataalamu wataka ushirikiano kuikabili TB
Uganda 'yacopy' na 'kupaste' kwa Wakenya