Benchi la Ufundi la KMC FC, limepanga mpango kazi maalum wa kuibamiza Young Africans katika mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22, utakaopigwa Jumanne (Oktoba 19) mjini Songea mkoani Ruvuma.

KMC FC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, huku wakiuchagua Uwanja wa Majimaji, kufuatia kanuni za Ligi Kuu kuruhusu kufanya vivyo.

Mpango maalum uliowekwa na Benchi la Ufundi la klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es salaam ni mazoezi maalum kwa wachezaji wao muhimu kama Miraj Athuman, Awesu Awesu,Juma Kaseja wamepewa program maalumu kwa ajili ya mechi zao zijazo ikiwa ni pamoja na ile dhidi ya Young Africans.

Afisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema tayari benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, John Simkoko na msaidizi wake Habib Kondo pamoja na Hamadi Ally wameanza kuufanyia mpango kazi huo kwa wachezaji wao.

“Maandalizi yameanza ambapo kwa sasa makocha wetu wametoa program maalumu kwa wachezaji wetu kikubwa ni kuona kwamba tunashinda mechi zetu zijazo ikiwa ni pamoja na ile dhidi ya Young Africans ambayo tutacheza Uwanja wa Majimaji, Songea.

“Hatujaanza vizuri msimu wa 2021/22 kwa kuwa mchezo wa kwanza tulipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania na mchezo wa pili tulilazimisha sare mbele ya Coastal Union hivyo tupo tayari kwa ajili ya ushindani,” amesema Mwagala.

Kwenye msimamo Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22, KMC ipo nafasi ya 15 baada ya kucheza michezo miwili, ikijikusanyia alama moja, kufuatia sare ya bila kufungana dhidi ya Coastal Union, huku ikitangulia kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania.

Mwakinyo azidi kutamba duniani
FIFA yaombwa kuiadhibu Real Madrid