Baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana dhidi ya Namungo FC Jumamosi (Oktoba Mosi), Kikosi cha KMC FC kimerejea na kuanza maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Ijumaa (OKtoba 07) katika uwanja wa Uhuru hapa Jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni, kilirejea jijini Dar es salaam jana Jumapili (Oktoba Pili), majira ya Alfajiri.

KMC FC inajiandaa na mchezo huo ambao ni wapili kuchezwa nyumbani kati ya michezo mitano ambayo imeshacheza hadi sasa, huku mikakati ni kuhakikisha wanazinyakua alama tatu muhimu, licha ya Ligi kuwa na ushindani mkubwa.

Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amsema wachezaji wote wamerejea wakiwa na Ari, Morali nzuri isipokuwa Ibrahimu Ame pamoja na Hance Masoud ambao waliumia kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC uliopigwa Uwanja wa Majaliwa Ruangwa Mkoani Lindi.

“ Tumerejea jana alfajiri kutoka Ruangwa, ambapo tulikuwa kwenye mchezo dhidi ya Namungo, tumerudi salama, na tulipumzika na leo tumeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo unaokuja dhidi ya Ruvu, tunafahamu ushindani wa mchezo huo namna ulivyo, lakini tutafanya maandalizi yetu vizuri kwakuwa malengo ni kupata alama tatu.”

“Kwenye ligi hivi sasa unapo kwenda kukutana na mpinzani wako, kila mmoja anakuwa amejipanga vizuri, na hii nikutokana na ushindani uliopo, hivyo na sisi kama Timu ya KMC tunajiandaa vema, mchezo upondani ya uwezo wetu na siku zote Timu bora haiwezi kukosa alama tatu muhimu mara mbili, tumekosa dhidi ya Namungo na sasa tunajipanga dhidi ya Ruvu Shooting.” amesema Christina

KMC FC hadi sasa ipo kwenye nafasi ya tisa ikiwa imecheza michezo mitano na kujikusanyia jumla ya alama sita na magoli sita ambapo michezo ambayo tayari imeshacheza ni dhidi ya Coast Union ya mkoani Tanga, Polisi Tanzania ya mkoani Kilimanjaro, Simba ya Jijini Dar es Salaam, Ihefu ya Mbarali mkoani Mbeya pamoja na Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi.

Aliyepindua nchi akutana na Baraza la Mawaziri, awapa agizo
Kocha Nabi afichua kumkataa Mwamnyeto