Kikosi cha Wachezaji 22 wa KMC FC, Viongozi pamoja na Benchi la Ufundi lao Ijumaa (Februari 03), imeondoka Jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Morogoro, tayari kwa mchezo wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa keshokutwa Jumapili (Februali 05) katika Uwanja wa Jamuhuri mkoani humo.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imeondoka baada ya kufanya maandalizi yake ya mwisho mapema asubuhi na wachezaji wote wameonesha kuwa tayari kukipiga katika Uwanja huo, ambao Ruvu Shooting wanautumia kwa sasa.

KMC FC chini ya Kocha Mkuu Thierry Hitimana inakwenda kwenye mchezo huo ikifahamu kuwa utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na kwamba kila mmoja anahitaji matokeo hasa ukizingatia Ligi inakwenda ukingoni kwa sasa.

Aidha KMC FC katika safari hiyo imewakosa Wachezaji muhimu wa nne kutokana na sababu za majeraha ambao ni Waziri Junior Shentembo, Daruweshi Saliboko, Awesu Ally Awesu pamoja na Matheo Anton.

“Tunakwenda kwenye mchezo mgumu tukiwa ugenini, tunafahamu umuhimu wa mchezo huo kwasababu tunahitaji matokeo mazuri na hata Ruvu Shooting nao wanayahitaji pia, hivyo kikubwa tunakwenda kupambana hadi dakika ya mwisho.”

“Ukiangalia kwenye mchezo wa mwisho KMC FC tulipoteza dhidi ya Namungo , matokeo ambayo yalimuumiza kila mmoja wetu, hivyo tunawaahidi mashabiki zetu kuwa pamoja na ugumu wa michezo tunayokutana nayo bado tutapambana kuhakikisha tunafanya vizuri.” amesema Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala

KMC FC inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imeshacheza jumla ya michezo 21 na hivyo kukusanya alama 23, huku ikishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara.

Mdhamini mpya Simba SC kuidhinishwa CAF
Jean Baleke: Kimataifa tutafika mbali