Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar Awadh Juma amempongeza Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Pappe Ousmane Sakho, kwa kuonyesha mchezo mzuri dhidi ya kikosi chake leo Alhamis (Juni 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Xar es salaam.

Sakho aliitanguliza Simba SC kwa kufunga bao maridadi la kuongoza, kabla ya mlinda lango Shaban Kado kufanya uzembe na kuruhusu mpira kuvuka mstari wa goli na kusababisha bao la pili kwa wenyeji.

Awadh amesema Sakho ameonyesha uhodari na ukomavu wa akili kwa kupambana dhidi ya safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar na kufanikiwa kufunga bao ambalo amekiri lilikua zuri na kiwango.

“Sakho ameonyesha uwezo mkubwa na kuisaidia timu yake, huu ni kama mchezo wa pili ama watatu anafunga bao kama hili, kwa hiyo upevu wa akili umeamua matokeo.”

“Wachezaji wangu hawakuwa makini na walijikuta wakifanya makosa yaliyopelekea kupoteza leo mbele ya Simba, ambayo tuliamini wangecheza kwa nguvu na kushambulia kwa kasi na ndivyo ilivyokuwa.” amesema Awadh Juma

Kwa ushindi wa mabao 2-0, Simba SC inafikisha alama 60 zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 70 kileleni.

Mtibwa Sugar yenye alama 31, imeendelea kushika nafasi ya 12 ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, kisha itamaliza msimu kwa kucheza na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC itamaliza michezo yake ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kisha watapambana na Mbeya Kwanza FC kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Matola: Beno Kakolanya apambane zaidi
Wakenya:Uhuru na Ruto ni 'sikio la kufa'