Mgogoro wa Chama Cha Wananchi (CUF) umeendelea kuchukua sura tofauti hususan wakati huu ambapo chama hicho kinajiandaa kufanya uchaguzi mdogo Januari 27 mwakani.

Mgogoro huo kati ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad umeendelea kuutafuna umoja wa chama hicho na kuathiri shughuli za kiutendaji huku kila upande ukirusha lawama kwa upande mwingine.

Kufutia sintofahamu ya kitakachotokea katika uchaguzi huo, baada ya kila upande kujipanga kuteua wagombea wake, Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya chama hicho, Julius Mtatiro amedai kuwa chama hicho hakiko tayari kushirikiana na Profesa Lipumba kwani ni mtu wa CCM.

“Hatuwezi kufanya kazi na mtu wa CCM,” Mtatiro anakaririwa na Mwananchi kuhusu Profesa Lipumba. “Kumleta karibu yetu ni kumleta atuharibie chama, jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu.” Aliongeza.

Mtatiro alidai kuwa maandalizi ya uchaguzi huo mdogo unaendelea vizuri na kwamba Katibu Mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu wa chama pamoja na Kamati za utendaji wanatimiza wajibu wao kuhakikisha wanapitisha wagombea.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alidai kuwa Ukawa wataendelea kumuunga mkono Maalim Seif na kwamba hawamtambui Profesa Ibrahim Lipumba.

Hata hivyo, Profesa Lipumba ameendelea kusisitiza kuwa hatakubali kukiacha chama hicho kiingie mikononi mwa Edward Lowassa (Waziri Mkuu Mstaafu) au kumezwa na Chadema badala yake atahakikisha anakipigania kwa maslahi ya wanachama wote kwa ujumla.

Profesa Lipumba pia amekuwa akimtaka Maalim Seif kupokea simu yake ili wazungumze na kumaliza mgogoro huo ili aendelee kumpangia majukumu kama ilivyokuwa awali.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliibua mgogoro mzito ndani ya chama hicho baada ya kutangaza kufuta barua yake ya kujiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti na kurejea ofisini akiidhinishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Baraza Kuu la chama hicho limefungua kesi dhidi ya uamuzi wa Msajili na kuiomba Mahakama kubatilisha uamuzi huo na kumtaka asiingilie maamuzi ya chama.

Baraza hilo lilitangaza kumvua uanachama Profesa Lipumba na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa sababu za kukihujumu na kuvuruga uchaguzi wa Mwenyekiti mpya uliokuwa ufanyike jijini Dar es Salaam.

Mgogoro wa uongozi wa chama hicho ambao tayari umeshatua Mahakama Kuu unatarajiwa kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo Disemba 14 mwaka huu.

Viongozi matumbo joto, ni baada ya mali zao kuanza kuchunguzwa
TPA yapokea msaada wa Bilioni132/- za upanuzi wa bandari