Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya, amezungumzia matukio ya hivi karibuni ya wabunge na viongozi wa vyama vya upinzani kutimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Lissu ambaye ni mwanasheria na mnadhimu mkuu wa Chadema, amemtaja aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbroad Slaa akieleza kuwa hakuna kipya kinachofanyika kwa kuzingatia historia ya siasa nchini.

“Watu hawafahamu historia au wanajisahaulisha. Lau Masha alitokea CCM, amerudi CCM, kuna cha ajabu?” Lissu amehoji.

“Mbunge wetu wa muda mrefu aliyekuwa katibu mkuu wa chama, Dkt. Slaa yuko wapi? Alihoji tena akisisitiza kuwa orodha ya mifano hiyo ni ndefu.

Dkt. Wilbroad Slaa

Lissu alieleza kuwa matukio ya kuhama vyama ni ya kawaida huku akiwataka wanachama na viongozi wa kambi ya upinzani wasikatishwe tamaa na hatua hizo.

Siku chache zilizopita, Maulid Mtulia, aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama Cha Wanachi (CUF), alitangaza kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM akieleza kuwa uamuzi wake umetokana na kuridhishwa na kazi inayofanywa na Rais John Magufuli.

Hatua ya Mtulia imekuja siku chache baada ya David Kafulila (aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini), Patrobas Katambi (aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema) na wengine waliokuwa viongozi waandamizi wa ACT-Wazalendo kutangaza kuhamia CCM.

Wakati CCM inavuna viongozi hao, Chadema ilimvuna aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

CUF yafunguka Mtulia kuhamia CCM
TBA yakiri majengo mapya ya UDSM kupata nyufa