Ni ngumu kuamini kichwa cha habari cha makala hii fupi, lakini kabla haujahukumu kitabu kwa kuangalia jarada lake pekee, jaribu kufuatilia mistari michache nitakayoiandika hapa.

Edward Lowassa, ni moja kati ya Mawaziri Wakuu wa zamani waliojiimarisha na kukubalika sana kwa utendaji wake huku akiwa na ushawishi mkubwa kuliko mwanasiasa yoyote wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne. Na ndiye Mgombea aliyeweka historia kubwa zaidi ya upinzani mzito dhidi ya CCM baada ya kuhamia Chadema na kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ingawa Lowassa alipata pigo kubwa baada ya kukumbwa na kashfa maarufu ya ufisadi wa mabilioni ya ‘Richmond’, iliyompelekea kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu mwaka 2008, matusi na kejeli alizokutana nazo bado hazikumyumbisha. Aliendelea kusema kile alichokiamini kuwa yeye hafaidika na fedha hizo. Katika kipindi fulani, aliamua kukaa kimya kwa muda huku akijipanga kimyakimya.

Wakati akiwa CCM, tafiti mbalimbali zilionesha kuwa ndiye aliyekuwa anakubalika zaidi kwa wananchi kati ya waliokuwa wakitajwa kuwania nafasi ya Rais (Dk. Magufuli hakudhaniwa wakati huo).

Lowassa alivunja ukimya Bungeni alipokuwa akitoa mchango wake akiukosoa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, huku akizungumzia uongozi autakao ambao utawafaa wananchi.

“Swala la nchi hii… mnazungumza hakuna utekelezaji. Tutazungumza lakini discipline (nidhamu) ya Malaysia ni tofauti. Hapa kuna uswahili mwingi, mnakaa mnaamua hamtekelezi,’ alisema.

“Kinatakiwa chombo ambacho kinaweza kufanya maamuzi magumu na yakawa maamuzi magumu yanayotekelezeka kwelikweli. Mkishakubaliana mambo yafanyike. Haiwezekani katika nchi, kila mtu akawa analalamika… kiongozi analalamika, wananchi wanalalamika, mtumishi wa serikali analalamika. Hatuwezi kuwa jamii ya kulalamika, lazima awepo mtu mmoja anayefanya maamuzi na kuchukua hatua. Bila kuchukua hatua tutaendelea kulalamikiana,” Lowassa alisema kwa msisitizo huku akipigiwa makofi mengi na wabunge.

Ingawa sina uhakika kama Rais Magufuli ambaye wakati huo alikuwa Mbunge na Waziri, alikuwa miongoni mwa waliompigia makofi, lakini kwa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza, bila shaka hizo ‘points’ aliziunga mkono.

Utekelezaji na maamuzi ya Rais Magufuli hususan ya hivi karibuni ukilinganisha na kauli ya Lowassa iliyokaririwa hapo juu, utakubaliana na mimi kuwa kiongozi aliyekuwa anapigiwa chapuo bungeni na Lowassa siku hiyo ni huyu tuliyenaye hivi sasa, mzee wa ‘Hapa Kazi Tu’.

Kama Lowassa alivyotaka kiongozi wa nchi hii awe, Rais Magufuli hapendi watu wanaolalamika. Juzi alidhihirisha hilo alipowapiga marufuku Makatibu Wakuu na Mawaziri kulalamika kuhusu fedha za matumizi mengineyo maarufu kama ‘OC’ (Other Charges). Alisema ametuma watu kuwarekodi mawaziri wanaolalamika na kwamba kama wanaona kiasi cha fedha wanazopewa kwa ajili ya OC hakitoshi basi waache kazi.

“Kuna mpaka Mawaziri wengine naona wanalalamika, nawatafuta… nimetuma watu wawarekodi, kwa sababu mindset yao bado haijabadilika. Wanafikiri bado tuko kwenye treni hiyohiyo. They will go,” alisema Rais Magufuli juzi, dakika chache baada ya kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela kwa kutoa taarifa zisizo za kweli kuwa hakuna watumishi hewa mkoani kwake.

Rais Magufuli amerudisha ‘discipline’ na kuondoa ‘uswahili’ alioutaja Lowassa wakati akichangia kwenye kikao cha Bunge.

Ingawa sio kwamba Lowassa anaunga mkono kila anachofanya Rais Magufuli, kama alivyodai hivi karibuni, lakini kuna mambo aliyoyataka na kuyabainisha wazi yanafanyiwa kazi kwa ufanisi na nguvu kubwa na Rais Magufuli.

Kwa hali hiyo, tunaamini kuwa katika uchaguzi uliopita, pamoja na mambo mengine, tulikuwa na wagombea wenye sifa za kufanya maamuzi magumu na kuondoa ‘uswahili’, ingawa lazima wanaziadiana kiwango cha kuchukua maamuzi hayo.

Rais Magufuli hakutarajiwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, lakini inawezekana Mungu alikuwa amemchagua japokuwa binadamu walishindwa kumuona akiwa katikati yao. Hata hivyo, Mungu alimpa ushindani mzito kutoka kwa Lowassa aliyekuwa anakubalika zaidi tangu zamani, ushindani huo umemuongeza nguvu katika utekelezaji wa majumu yake.

Hii Ndio Orodha Ya Wanasoka Tajiri Duniani
Young Africans, Azam FC Wataka Game Zao Zisogezwe Mbele