Zikiwa zimebaki siku kumi za lala salama kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambapo zitahitimishwa baada ya watanzania kupiga kura Oktoba 25, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa amesema hakuna mtu atakayeweza kuwazuia kuleta mabadiliko.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika mkoani Kagera. Alimpongeza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine kwa kuimarisha Chadema na kudai kuwa chama hicho sasa kimekomaa na kiko tayari kuingia Ikulu.

“Basi la mabadiliko liko katika kasi ya ajabu, hakuna wa kutuzuia,” alisema Lowassa.

Aidha, aliitumia nafasi hiyo kumpongeza Balozi Juma Mwapachu kwa uamuzi wake wa kuihama CCM na kujiunga na harakati za mabadiliko akidai kuwa hiyo ni heshima kubwa kwake.

“Balozi Mwapachu ni mwanadiplomasia aliyekamilika na msomi, kujiunga kwake na harakati zangu ni heshima. Inathibitisha pia kuwa tunachokifanya hapa Ukawa ni kitu muhimu sana,” alisema.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliwaomba wananchi hao kumpigia kura za ndio ili awe rais wa Tanzania akiahidi kuwa atahakikisha anaongeza ajira hasa kwa vijana kwa kuwapa elimu na kuwakopesha mitaji ili waweze kutumia elimu yao kujiajiri.

Pia, alieleza kuwa ataongeza idadi ya vijana wanaojiunga na JKT na kuongeza muda wa mafunzo stadi katika jeshi hilo ili vijana hao waweze kujiajiri pindi wanapomaliza mafunzo hayo.

Valdes Kupigwa Bei Januari 2016
Mwapachu Arudisha Rasmi Kadi Ya CCM