Milio ya Mabomu ya Mchozi na kile linachoaminika kuwa ni magurunedi ya kurusha kwa mkono yaliwaamsha wakazi wa mji wa Moshi jana ikiwa ni sehemu ya mazoezi ya Jeshi la Polisi.

Taarifa kutoka mjini humo zimeeleza kuwa magari mengi ya jeshi la polisi pamoja na polisi wa vikosi vya kawaida na FFU, askari wa usalama barabarani na vikosi vingine vya kawaida walisambaa karibu kila kona ya manispaa hiyo wakifanya ‘patrol’.

Hali ya vikosi vya jeshi la polisi kuonekana mitaani wakiwa na silaha imeonekana pia katika mikoa mingine kama Iringa na Singida yakiambatana na mazoezi makali yanayoonekana kufanywa na vikosi vya jeshi hilo.

Polisi 2

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limewatuliza wananchi wote nchini kuwa kinachoonekana ni sehemu ya mazoezi ya kawaida tu ya Jeshi hilo na kwamba wasiwe na hofu kwani hayalengi kuzuia kikundi chochote kinachofanya shughuli halali.

“Watu hawapaswi kuhamaki,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi. “Haya ni mazoezi endelevu ya kawaida. Huwa tunayafanya katika eneo la Kihesa lakini hivi sasa tumeamua kubadili eneo la mazoezi. Sasa tupo Mwembetogwa,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi hilo limeeleza kuwashikilia watu wawili katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro kwa kosa la kuuza fulana zenye maandishi ya Operesheni ya Chadema iliyoewa jina la UKUTA, maandishi yaliyotajwa kuwa ya kichochezi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro amewataka wananchi kutokuwa na hofu na kuondelea na shughuli zao kwani hakuna mtu atakayeandamana Septemba 1.

Kamanda Siro pia amewataka wananchi wote kutii sheria bila shuruti na kujiepusha na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Viongozi wa Chadema wametaja hatua hiyo kama sehemu ya kuwatishia wanachama wao kutoshiriki maandamano huku wakisisitiza kuwa hawataacha kuandamana Septemba 1.

“Tunawahakikishia hatutarudi nyuma pale katiba na haki ya kidemokrasia inapochezewa au kuwa chini ya mtu fulani,” alisema Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Edward Lowassa.

“Najua Polisi watapiga watu, wataumiza watu na hata kuua. Lakini niwahakikishie tu kwamba wao na walio na Mamlaka wataishia katika Mahakama ya Kimataifa,” aliongeza.

Chanzo: The Citizen

Serikali kufikisha umeme Mlele, Katavi novemba, na nchi nzima
Waliokula fedha za Chama cha ushirika kuchukuliwa hatua, Katavi