Madereva wa matipa ya mchanga , wanaotumia barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro,  wamefanya mgomo wa kulalamikia wakala wa barabara (TANROADS) mkoani Pwani, unaowakamata kutokana na kutofunga mchanga vizuri na kuwapiga faini ya sh.500,000.

Madereva hao waliweka mgomo huo katika eneo la Tamco ambapo ndipo watendaji wa wakala huo walikuwa wakiwasimamisha kwa ajili ya kukagua wale waliojaza mchanga hali inayosababisha kuchafua miundombinu ya barabara.

Dereva Martine Magari na Emmanuel Shao, walisema ni kweli wapo madereva wasiofunga vizuri maturubai ya magari yao lakini tatizo kubwa ni kukosa elimu ya kufunga kwa ubora .

Shao aliziomba idara na mamlaka husika kutoa elimu juu ya sheria mbalimbali kwani inakuwa sio rahisi kuelewa sheria zote zinazotungwa bila kupatiwa elimu ya kutosha.

Kwa mujibu wa kaimu meneja TANROADS mkoani Pwani, Injinia Yudas Msangi, alisema wapo kwenye operesheni ya kukagua magari kwa kufuata sheria ya barabara ya mwaka 2007 namba 13 kifungu namba 46C, inayokataza kuchafua barabara .

Alisema kuwa hakuna anaewaonea madereva hao, kwani wanatambua vilivyo kuhusu sheria hiyo na mara kwa mara huwa wakielimishwa kuacha tabia ya kuzembea kufunga mchanga vizuri na kuongeza kuwa , wanatoa muda hadi jumatatu ijayo zoezi hilo litaendelea ili kudhibiti uchafuzi huo wa miundombinu ya barabara.

Awali kamanda wa usalama barabarani, Abdi Issango ,alifika eneo la tukio na kuzungumza na madereva hao  na uongozi wa tanroads mkoa,akiwemo kaimu meneja, msaidizi wake pamoja na meneja wa barabara mkoa mama Urio.

 

Alisema ni kweli madereva wengi wamekuwa hawafungi vizuri mchanga kwa kutumia kifungio (hooks) kwenye maturubai ili kuzuia mchanga usimwagike.

Baada ya kamanda huyo kuzungumza na pande hizo mbili ,madereva hao walitawanyika na kuridhia maelekezo waliyopatiwa sambamba na kukubaliana kuanza kwa zoezi hilo wiki ijayo.

Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi mkoani Simiyu
Mbunge wa Chalinze Akabidhi Magodoro 200 Shule ya Sekondari Moreto