Madiwani wa jiji la Dar es Salaam wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, jana walifika katika ofisi ya Mkurugenzi wa jiji kushinikiza ofisi hiyo kukamilisha zoezi la uchaguzi wa Meya wa jiji hilo unaopigwa danadana kila unapopangwa kufanyika.

Mwenyekiti wa madiwani na wabunge wa Ukawa jijini Dar es Salaam, Manase Mjema akiwa nje ya ofisi ya Mkurugenzi wa jiji hilo, alisema kuwa lengo lao ni kushinikiza kupewa majibu ya lini uchaguzi wa Meya utaitishwa kwani kuna maamuzi yaliyopaswa kufanywa na Meya yanafanyika hivi sasa bila uwepo wa Meya husika na jopo lake.

“Tunachohitaji ni kufahamu lini wataitisha kikao cha kumchagua Meya wa jiji la Dar es Salaam. Kwa sababu kuna mambo ambayo yanaendeshwa katika jiji hili sasa hivi ambayo Meya angekuwepo yangeenda vizuri. Kwa sababu kuna mambo ambayo yanaendeshwa bila Meya. Sasa sijui yanaendeshwa kwa sheria zipi.“Ingetakiwa sasa hivi Meya wa Jiji awe na kikosi chake ili waweze kuendesha mambo ya jiji,” alisema Mjema.

Uchaguzi wa kumpata Meya wa jiji hilo umekuwa ‘kitendawili’ hususan kufuatia kuahirishwa mara kwa mara huku ukizua migogoro na vurugu zilizopelekea kukamatwa kwa baadhi ya wabunge na madiwani wa vyama vinavyounda Ukawa jijini humo.

Februari 27 mwaka huu, Mkurugenzi wa Jiji hilo alitangaza kuahirisha uchaguzi wa Meya uliokuwa umepangwa kufanyika siku hiyo na kueleza kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kuwepo pingamizi la mahakama kufuatia kesi iliyofunguliwa na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi.

Hata hivyo, siku chache baadae, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikana kutoa zuio lolote la uchaguzi huo huku ikibainisha kuwa aliyesema hivyo alipotosha.

Wamiliki wa Jamii Forum watinga mahakamani
Zanzibar Kuwa Mwenyeji Mashindano Ya 11 Ya Judo Ya Afrika Mashariki Na Kati