Kazi ya utumbuaji wajipu aliyojipa Rais John Magufuli inaendelea kupata wateja zaidi baada ya jana Mkaguzi Mkuu, Mussa Assad kumkabidhi ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano ya Ikulu, CAG, Mussa Assad alimkabidhi Rais Magufuli ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mujibu wa Sheria inayomtaka kufanya hivyo kabla ya mwisho wa mwezi Machi.

Historia inaonesha kuwa ripoti za ukaguzi ya CAG hubaini uozo mwingi kwenye taasisi za umma, ufisadi, ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka ambavyo katika serikali ya awamu ya Tano vimepewa jina la ‘Majipu’.

Rais ataipitia taarifa hiyo kabla ya kulikabidhi Bunge kwa ajili ya kujadiliwa katika Mkutano wa tatu utakaofanyika mjini Dodoma kuanzia Aprili 19 mwaka huu.

Taarifa hiyo ya ikulu imeeleza kuwa Rais Magufuli amempongeza CAG na timu yake kwa kuandaa ripoti hiyo muhimu.

“Ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi. Ameahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi zake,” taarifa ya Ikulu imeeleza.

 

Mbowe awataja watakaokula matunda ya Kazi ya Lowassa Chadema
Dk. Shein aanza kupanga safu yake, Amteua Balozi Seif Ali kushika nafasi hii