Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora, Samwel Sitta

Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.

Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za kifo cha mzee Sitta kwa mshtuko na masikitiko makubwa kwani taifa limepoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.

Amesema atamkumbuka mzee Sitta kwa uchapaji kazi wake, uzalendo na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbali mbali za siasa na Serikali.

Rais ametoa pole kwa mke wa marehemu, Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa jimbo la Urambo na familia nzima ya marehemu, ametoa po0le pia kwa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Urambo na mkoa wa Tabora pamoja na watu wote walioguswa na msiba huo.

Rais amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.

Al Masry Wachafua Hali Ya Hewa Zamalek SC
Takukuru yazipekua tuhuma za rushwa ya Milioni 10 kwa wabunge wa CCM